IQNA

Utawala wa Aal Khalifa ndio unaohusika na kuzorota kwa hali ya afya ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Haq

18:00 - October 15, 2011
Habari ID: 2205229
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya nchini Bahrain amesema kuwa utawala wa kifalme wa Aal Khalifa ndio unaohusika moja kwa moja na kuzorota kwa hali ya kiafya ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Haq na kuutaka utawala huo kuwajibika kuhusiana na suala hilo.
Ikimnuku Ayatullah Sheikh Isa Qassim, khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Bahrain ambaye pia ni kiongozi wa Mashia waliowengi wa nchi hiyo, tovuti ya chama cha upinzani cha al-Wifaq imesema kuwa utawala wa Aal Khalifa ndio unaobeba jukumu la kulinda usalama wa Hassan Musheima' mmoja wa wabunge wa nchi hiyo wanaoteswa kizuizini.
Ayatullah Isa Qassim amesema kwamba mbunge huyo ni mmoja wa wanamapinduzi mashuhuri wa taifa la Bahrain na kwamba utawala wa Aal Khalifa unapaswa kubebeshwa lawama za kuzorota hali yake ya afya kwenye jela.
Amesema kwamba hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kumzuia Musheima' apate matibabu ni sababu kuu inayozorotesha afya yake na kwamba serikali hiyo inapaswa kuwajibishwa kisheria kuhusiana na suala hilo.
Ameashiria hatua ya baadhi ya wanazuoni vibaraka ya kuharamisha maandamano halali ya kulalamikia dhulma na uonevu dhidi ya serikali na kuwataja wanazuoni hao kuwa maadui wakubwa zaidi wa dini ya Uislamu na kuongeza kuwa wanazuoni hao wanavunjia heshima taifa la Bahrain na wakati huohuo kuunga mkono dhulma ya watawala dhalimu wa nchi hiyo.
Ayatullah Isa Qassim amesema kuwa hivi sasa kuna lugha mbili zinazozungumzwa katika Mashariki ya Kati moja ikiwa ni ya serikali dhalimu zinazotumia jeshi na vyombo vya propaganda dhidi ya wananchi, na ya pili ni ya wananchi wanaopinga dhulma na uonevu na kwamba hatimaye ni lugha ya wananchi ndiyo itakayosikika zaidi na kupata ushindi wa mwisho. 879854
captcha