Mufti Mkuu wa Syria amesema kuwa serikali ya nchi hiyo inapigwa vita na madola ya Magharibi kwa ushirikiano wa vibaraka wao wa Kiarabu kutokana na uungaji mkono wake wa moja kwa moja kwa harakati za mapambano ya Kiislamu katika Mashariki ya Kati na masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu na hasa kuhusu suala la Palestina.
Akizungumza hivi karibuni mbele ya wasanii, wanafikra, watafiti na wanasiasa wa Kiislamu huko mjini Damascus, Mufti Ahmad Badrudeen Hassun amesema kuwa ni wazi kwamba Syria inakabiliwa na mashinikizo makubwa ya nchi za Magharibi kutokana na msimamo wake thabiti wa kuunga mkono harakati za mapambano ya Kiislamu na kujaribu kuvunja njama zilizoandaliwa vyema na madola hayo kwa shabaha ya kuvunja umoja na mshikamano wa nchi za Mashariki ya Kati.
Amesema Rais Bashar Assad wa Syria amekuwa akifanya juhudi kubwa za kufanya marekebisho na maendeleo nchini lakini maadui wamekuwa wakimsababishia matatizo mengi ya ndani ili kuvuruga juhudi hizo. Amesema maadui wa nchi hiyo wamekuwa wakitekeleza njama nyingi dhidi ya nchi hiyo ili kupata fursa ya kuidhibiti na kuiendesha wanavyotaka.
Mufti wa Syria amewataka wasomi na wanafikra wote duniani kutohadaika na propaganda zinazoenezwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na vya vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati, na kuwataka wasafiri nchini Syria ili kujiona wenyewe kwa karibu uhalisi wa mambo ya nchi hiyo. 881631