IQNA

Naibu mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Bahrain atiwa nguvuni

15:00 - October 19, 2011
Habari ID: 2208060
Askari usalama wa Bahrain jana Jumanne walimtia nguvuni Bi Jalila as-Salman, Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Bahrain.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Alam, askari hao walivamia nyumba ya bibi huyo katika mtaa wa Sahla na kumtia nguvuni kwa mara ya pili. Awali utawala wa Aal Khalifa ulikuwa umemhukumu mwalimu huyo kifungo cha miaka mitatu jela.
Wakili wa mwalimu huyo amesema kuwa askari usalama wa Bahrain wamemtia tena nguvuni mwalimu huyo wa Jumuiya ya Walimu wa Bahrain katika hali ambayo mahakama ya rufaa bado haijajibu ombi lake la kutaka kutazamwa upya hukumu iliyotolewa dhidi yake.
Bi as-Salman amesema kuwa askari usalama hao walivamia nyumba yao saa tisa usiku na kutaka kuvunja mlango wa nyumba hiyo lakini baba yake alitambua nia yao mapema na kufungua mlango kabla haujavunjwa. Askari hao walimchukua bibi huyo bila kumfahamisha sababu ya kumtia tena nguvuni.
Kabla ya hapo Bi Jalila alikamatwa na kuzuiwa katika kituo cha polisi cha Isah kwa muda wa siku 149. 882851
captcha