IQNA

Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi latakiwa kubuni sheria ya kupinga ubaguzi wa kimadhehebu

16:53 - October 23, 2011
Habari ID: 2210289
Allama Sheikh Hussein al-Mustafa, mhadhiri katika kituo cha kidini cha Qatif na Imam wa Ijumaa wa mji huo wa Saudia Arabia amelitaka Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lipitishe sheria ambayo itapiga marufuku ubaguzi wa kimadhehebu katika nchi wanachama.
Amesema kuwa hisia na siasa za ubaguzi wa kimadhehebu zimekuwa zikienea kwa kasi ya kutisha katika nchi wanachama wa baraza hilo na hivyo kuna udharura wa baraza hilo kubuni sheria ambazo zitapiga marufuku mwenendo huo.
Amesema kupitishwa kwa sheria kama hiyo kunalazimu kufanyiwa marekebisho makubwa miundo ya kiutawala na kuimarisha moyo wa umoja wa kitaifa katika nchi husika.
Mwanafikra huyo wa Kishia nchini Saudi Arabia amesema kuwa vyombo vya sheria vya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi vinapasa kutoa dhamana ya kutekelezwa sheria hiyo ili kuifanya kuwa na maana ya utendaji. Amesema wanazuoni na wahuburi wote wa kimadhehebu wanapaswa kulazimika kuzingatia misingi ya maadili na kulinda umoja wa kitaifa wa nchi za Kiislamu.
Mwanafikra huyo wa amekosoa vikali matamshi ya matusi yaliyotolewa hivi karibuni na al-Hudheifi, hatibu wa Msikiti wa Mtume (saw) dhidi ya Mashia na kusema kuwa kutolewa kwa matusi kama hayo kwenye mimbari ya Mtume kutawashajiisha Mawahabi wengine wenye misimamo ya kupindukia mipaka waenedelee kutoa matamshi kama hayo ya dharau dhidi ya Waislamu.
Imam huyo wa Qatif amesisitiza udharura wa kufutwa mbinu za kuwakufurisha Waislamu katika mifumo ya mafunzo ya baadhi ya nchi za Kiislamu na hasa Saudi Arabia na kuongeza kuwa mifumo hiyo inapasa kubadilishwa na mifumo ya mafunzo ya upendo, kuvumiliana kifikra na kiitikadi pamoja na kuishi pamoja kwa amani wafusia wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu.885046
captcha