IQNA

Utumiaji wa nara za kidini katika uchaguzi wa Misri wachunguzwa

15:38 - October 24, 2011
Habari ID: 2211008
Nara inayotumiwa na Chama cha Uadilifu na Uhuru kinachofungamana na harakati ya Ikhwanul Muslimin inayosema kuwa 'Uislamu ndio Suluhisho' ilichunguzwa jana Jumapili mjini Cairo na Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi inayoongozwa na Hani Mahmoud, ikiwa ni katika juhudi zake za kutayarisha mazingira ya kufanyika uchaguzi wa bunge ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao wa Novemba.
Muhmoud amesema kuwa licha ya kuwepo marufuku ya kutumiwa nara za kidini katika kampeni za uchaguzi huo lakini bado Chama cha Uadilifu na Uhuru kinasisitiza kuendelea kutumia nara hiyo katika kampeni zake na kwa hivyo suluhisho la jambo hilo linapasa kupatika kabla ya kuanza uchaguzi.
Vyama vya utaifa na vinavyopinga Uislamu vya Misri vimekuwa vikitoa mashinikizo makubwa dhidi ya kamati hiyo ili ikibane chama cha Ikhwanul Muslimin kisitumie nara za Kiislamu kwenye uchaguzi ujao kwa sababu jambo hilo linaweza kukifanya kipate ushindi mkubwa katika uchaguzi huo.
Hii ni katika hali ambayo chama hicho ambacho ni mrengo wa kisiasa wa Ikwanul Muslimin kinasisitiza kwamba utekelezaji wa sheria za Kiislamu ndilo suluhisho la pekee la matatizo mengi yanayoikumba Misri.
Awali Abdul Muizz Ibrahim, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Misri alitishia kwamba angefuta majina ya wagombea wote wanaotumia nara za kidini katika kampeni zao za uchaguzi. 885492
captcha