IQNA

Vyama vya Lebanon vyasisitiza udharura wa kufuatiliwa hatima ya Imam Musa Sadr

18:08 - October 25, 2011
Habari ID: 2211745
Jumuiya ya Vyama, Wafuasi na Shakhsia wa Kitaifa wa Lebanon imetoa taarifa ikiitaka serikali ya nchi hiyo ifuatilie kwa karibu suala la hatima ya Imam Musa Sadr aliyetekwa nyara nchini Libya na utawala wa dikteta Muammar Gaddafi, kama suala la kitaifa.
Mkuu wa Idara ya Uratibu ya jumuiya hiyo amesema kwamba serikali ya Beirut inapasa kufuatilia kwa karibu suala la kutekwa nyara Imam Sadr pamoja na wenzake wawili Sheikh Muhammad Ya'qub na Abbas Badrudeen na kulipa suala hilo umuhimu wa kitaifa.
Taarifa hiyo imelaani vikali uingiliaji wa kijeshi wa Nato katika masuala ya Libya na kuendelea kuwepo askari wake katika ardhi ya nchi hiyo. Imesema kuwa Nato inafanya juhudi za kurejesha Libya ukoloni mamboleo, kupora utajiri wa nchi hiyo pamoja na kubuni mfumo wa utawala ambao utadhamini maslahi ya nchi za Magharibi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Taarifa ya jumuiya hiyo inaendelea kusema kuwa Libya imeingia katika awamu mpya ya kisiasa baada ya kuanguka utawala wa Muammar Gaddafi na kuitaka mirengo ya kisiasa na kitaifa ya nchi hiyo kupanga sera ambazo zitakabiliana na ukoloni wa nchi za Magharibi nchini Libya na kutayarisha mazingira ya kuimarishwa uhuru na kujitawala nchi hiyo.
Taarifa hiyo ya vyama vya kitaifa vya Lebanon imewataka Walibya kubuni mfumo huru wa kitaifa ambao hautategemea madola ya Magharibi, na kutetea masuala ya Kiarabu na hasa suala la Palestina na mapambano dhidi ya uchokozi na kujipanua utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Waarabu. 886793
captcha