IQNA

Gaddafi azikwa kwa mujibu wa fatuwa ya Mufti wa nchi hiyo

17:36 - October 25, 2011
Habari ID: 2211747
Mustafa Abdul Jalil, Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Libya ametangaza kwamba dikteta Muammar Gaddafi wa nchi hiyo alizikwa jana Jumatatu katika sehemu isiyojulikana, kwa mujibu wa fatuwa iliyotolewa na Baraza Kuu la Mamufti wa Libya.
Kwa mujibu wa gazeti la Kiarabu la al Quds al-Arabi linalochapishwa mjini London Uingereza, dikteta huyo wa zamani amezikwa sehemu isiyojulikana katika mojawapo ya majangwa ya nchi hiyo. Amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya miili ya dikteta huyo, mwanawe Mu'tasim na Abu Bakr Yunus Jabir aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Qaddafi kuanza kuoza na kutoa harufu isiyovumilika, na hivyo kutoruhusu tena watu kuendelea kushuhudia maiti zao.
Awali Sheikh as-Swadiq al-Gharyani Mufti wa Libya alitoa taarifa akiharamisha kusaliwa swala ya maiti mwili wa Gaddafi na kusema kuwa jambo hilo linajuzu tu kwa familia yake. Amesema haijuzu kwa Waislamu, wanazuoni na maimamu wa misikiti kuswalia swala ya maiti jeneza la Gaddafi kwa sababu alikuwa kafiri moja kwa moja aliyepinga suna za Mtume (saw).
Mufti wa Libya amesema sera na tabia zake katika miaka ya hivi karibuni zinabaini wazi kuwa alikuwa ametoka nje ya misingi ya Uislamu.
Mufti huyo amesema kuwa kaburi la Gaddafi linapaswa kuzuiwa kuwa sehemu ya kuzuriwa na Waislamu na kubadilishwa kuwa chanzo cha fitina miongoni mwa Walibya. 886881
captcha