IQNA

Mufti wa Misri: Tutakata mikono ya watu wanaojaribu kuvunjia heshima makaburi ya Maimamu wa Mashia

15:43 - October 31, 2011
Habari ID: 2215201
Ali Jumua, Mufti wa Misri amewatahadharisha watu wanaojaribu kuharibu makaburi ya Maimamu wa Mashia ambao ni Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kusisitiza kwamba Waislamu watakata mikono ya watu hao wanaojaribu kuharibu kaburi au kwa ibara nyingine, maqaam ya Imam Hussein (as).
Mufti Jumua amesema kwamba anapinga vikali wito unaotolewa na baadhi ya watu, wa kutaka kuharibu makaburi ya Ahlul Beit wa Mtume (saw), mawalii na wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu na kuongeza kuwa wito huo unatolewa na watu wapotofu wanaojaribu kuharibu jina la Uislamu kutokana na misimamo yao ya kupindukia mipaka.
Mufti wa Misri amesema Mtume Mtukufu aliwafundisha Waislamu kuwa kukosea heshima baadhi ya makaburi, maziara na haram za watukufu wa kidini ni kutoka kwenye misingi ya dini, akili na utu na kwamba kila mtu anayefanya kitendo hicho huwa ni jahili asiyejua lolote katika dini.
Amesema anashangazwa na baadhi ya watu wanaowakufurisha Waislamu wenzao na kuyataja makaburi ya Ahlul Beit (as) kuwa ni masanamu katika hali ambayo kaburi la Mtume (saw) mwenyewe limesimama imara huko katika mji mtakatifu wa Madina.
Vilevile amelaani vikali watu wanaotoa wito wa kuharibiwa kaburi la Imam Hussein (as) na kuwaambia Mawahabi wanaotoa wito huo kuwa ni majahili ambao hawafahamu lolote katika dini. 890449
captcha