Ofisi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulamaa wa Ahlusunna huko kusini mwa Iraq imetoa taarifa ikilaani hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ya kusimamisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo na kusema, jumuiya hiyo inawaunga mkono vibaraka na watu wenye misimamo ya kupindukia.
Sheikh Khalid al Mulla amesema katika taarifa hiyo kuwa Arab League ina misimamo ya kindumakuwili kuhusu masuala ya ulimwengu wa Kiarabu na kuongeza kuwa jumuiya hiyo imekuwa na misimamo isiyokuwa sahihi kuhusu hali ya sasa katika Mashariki ya Kati.
Sheikh al Mulla ameongeza kuwa Arab League imepuuza kabisa na kunyamazia kimya hali ya wananchi madhlumu wa Bahrain ambao wanauawa na kukandamizwa na utawala wa Aal Khalifa.
Sheikh Khalid al Mulla amesema kuwa uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kusimamisha uanachama wa Syria haukuwa sahihi hususan kwa kutilia maanani misimamo ya serikali ya Damascus ya kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina na Lebanon dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Vilevile amelaani makundi yenye misimamo mikali yaliyotumwa nchini Syria kwa ajili ya kuvuruga amani na utulivu na kupinga aina yoyote ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. 899268