Kamal Halbawi ambaye alikuwa katika maandamano ya wananchi kwenye Medani ya Tahrir mjini Cairo amesema kosa kubwa zaidi la wanamapinduzi wa Misri waliomiminika kwa wingi na kuung'oa madarakani utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak, ni kutochagua kiongozi wao mmoja na kuliamini Baraza la Kijeshi.
Amesisitiza kuwa wanamapinduzi wa Misri wanapaswa kuchagua kiongozi mmoja atakayewawakilishi katika mazungumzo na Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo na kuongeza kuwa, wanamapinduzi hao hawakupaswa kuliamini Baraza hilo la Kijeshi.
Bwana Halbawi ameyataka makundi yote ya vijana kumchagua kiongozi mmoja na akasema kuwa njia pekee ya kujiondoa katika mgogoro na changamoto ya sasa ni kuafikiana juu ya kiongozi mmoja ambaye atawasilisha matakwa ya wananchi kwa wanajeshi wanaotawala.
Msemaji wa zamani wa Ikhwanul Muslimin amesema taifa la Misri linapaswa kuwa na nafasi muhimu katika maamuzi yote ya nchi na katika kuteuwa serikali mpya.
Kamal Halbawi amesema iwapo vijana wa Misri wataendeleza maandamano yao kwa siku tatu hadi nne zijazo, wanajeshi wanaotawala nchi watalazimika kuacha kuingilia masuala ya kisiasa ya nchi hiyo. 903065