IQNA

Marufuku ya vazi la hijabu kwa watangazaji wa kike yafutwa Misri

16:56 - November 29, 2011
Habari ID: 2231467
Mahakama ya Masuala ya Kiidara ya mji wa Alexandria nchini Misri imefuta na kubatilisha marufuku ya vazi la hijabu la wanawake wa Kiislamu iliyokuwa imewekwa na Waziri wa Habari wa serikali iliyong'olewa madarakani ya Hosni Mubarak.
Mahakama hiyo pia imeamuru mtangazaji wa kike wa televisheni ya taifa ya Misri aliyekuwa amezuiwa kutangaza kwa sababu ya vazi lake la hijabu Maha al Shafi'i alipwe fidia ya pauni elfu 20 za Misri.
Mwaka 2008 Maha al Shafi'i mtangazaji wa kanali ya tano ya televisheni ya serikali ya Misri aliachishwa kazi na Waziri wa Habari wa wakati huo wa serikali ya dikteta Hosni Mubarak kwa sababu ya vazi lake la hijabu ya Kiislamu. Wakati huo mtangazaji huyo aliwasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya Waziri wa Habari na kutaka alipwe fidia kutokana na kwamba amri hiyo inakiuka katiba ya nchi.
Baada ya kung'olewa madarakani utawala wa dikteta Mubarak Mahakama ya Alexandria ilishughulikia kesi hiyo na hatimaye imetoa amri ya kufutwa marufuku ya vazi la hijabu kwa watangazaji wa kike.
Mahakama ya Masuala ya Kiidara ya Alexandria imetangaza kuwa vazi la hijabu linalinda heshima na utukufu wa mwanamke wa Kiislamu anayeheshimu mafundisho na thamani za dini hiyo tukufu na wala halimdunishi mbele ya watazamaji.
Taarifa ya mahakama hiyo imesema kupiga marufuku vazi la hijabu katika eneo lolote lile ni kukiuka uhuru wa mtu binafsi na kubana uhuru wake wa kifikra na kiitikadi. Imesisitiza kuwa watu wote waliopatwa na madhara kutokana na marufuku hiyo wanapaswa kulipwa fidia. 907889


captcha