IQNA

Mimbari za Imam Hussein (as) ni nguzo muhimu za kuhuishwa Ashura

16:32 - December 03, 2011
Habari ID: 2233468
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya nchini Bahrain amesisitiza kuwa mimbari za Imam Hussein (as) ni nguzo muhimu za kuhuisha hamasa na mapambano ya Imam huyo Mtukufu.
Akizungumza hapo jana Ijumaa katika Msikiti wa Imam Swadiq (as) nchini Bahrain Ayatullah Sheikh Isah Qassim amesema kuwa msingi wa kuhuishwa Ashura ni kufanyika maombolezo mazuri na ya kutoa mwamko kuhusiana na mapambano ya Imam Hussein (as) na wafuasi wake wachache mashujaa na wa kujitolea mhanga. Amesema maombolezo mengine yanayokwenda kinyume na jambo hilo na kupinga misingi ya sheria za Kiislamu hayana maana yoyote.
Akigusia matukio ya kisiasa ya Bahrain, Ayatullah Isah Qassim amesema kuwa wananchi shupavu wa Bahrain wanasisitiza juu ya udharura wa kupinduliwa mfumo wa utawala wa nchi hiyo na kwamba bila shaka matakwa yao yatatetkelezwa. Mwanazuoni huyo wa Bahrain amesema kuwa maslahi ya kitaifa hayapasi kugongana na misingi ya dini, akili wala thamani zinazokubalika na jamii na zilizosimama juu ya msingi wa mantiki.
Amelaani mauaji, ukandamizaji, vifungo vya dhulma dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na uvunjiwa heshima misikiti na kuongeza kuwa kamati iliyobuniwa hivi karibuni na utawala dhalimu wa Aal Khalifa kwa ajili ya kuchunguza matukio ya hivi karibuni nchini humo haina faida yoyote kwa sababu inaendesha uchunguzi wake kwa maslahi ya utawala huo.
Ayatullah Qassim Amesema badala ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo kamati hiyo inauvuruga na kuufanya kuwa mgumu zaidi. Amesema kubadilishwa misikiti na kuwa sehemu ya kutekelezewa jinai dhidi ya Waislamu na Uislamu ni kosa kubwa lisilosameheka wala kufumbiwa macho. 909762
captcha