IQNA

Amnesty International yailaumu Saudia kwa kukiuka haki za Mashia

16:54 - December 03, 2011
Habari ID: 2233486
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeilaumu Saudi Arabia kwa kupuuza haki za Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo na kutangaza kuwa utawala wa kifalme wa Riyadh umewatia mbaroni zaidi ya Mashia 300 kwa sababu ya kushiriki katika maandamano ya amani.
Amnesty International imeikosoa Saudi Arabia kwa kukiuka haki za binadamu na kusisitiza kuwa rasimu ya sheria ya kupambana na ugaidi inayotayarishwa nchini humo itazidisha ukandamizaji wa vyombo vya dola dhidi ya wapinzani wa serikali ya Riyadh.
Taarifa iliyotolewa jana na Amnesty International imesema serikali ya Saudia imekuwa ikikandamiza kwa kiwango kikubwa harakati za amani za wananchi kwa kutumia kisingizio cha kulinda amani.
Awali ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu ilisema kuwa Saudia imewakandamiza watu wanaoandamana kwa amani wakitaka marekebisho ya kisiasa na kwamba ukandamizaji huo wa kutisha unafanana na ule unaofanywa na serikali ya kifalme ya Riyadh dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya kigaidi.
Amnesty imesisitiza kuwa maelfu ya watu wameswekwa jela bila ya tuhuma wala kufikishwa mahakamani na kwamba mateso na muamala mbaya umekithiri sana nchini Saudi Arabia.
Ripoti hiyo pia imesema kuwa jeshi la Saudia limefanya mashambulizi makubwa katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo na kuwakamata mamia ya waandamanaji wengi wao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mwezi uliopita pekee Waislamu wanne wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi ya Saudi Arabia. 909469


captcha