IQNA

Baraza la Waislamu Ufaransa lalaani mpango wa marufuku ya hijabu

17:47 - December 07, 2011
Habari ID: 2235010
Baraza la Waislamu wa Ufaransa limetoa taarifa likilaani mpango uliowasilishwa katika Baraza la Seneti la nchi hiyo wa kupiga marufuku vazi la hijabu ya Kiislamu katika vituo vya starehe na michezo na shule za chekechea.
Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu wa Ufaransa Muhammad Mussawi amesema katika taarifa hiyo iliyotolewa jana kuwa Waislamu wana wasiwasi mkubwa kuhusu upasishwaji wa rasimu hiyo na kusisitiza kuwa kupiga marufuku vazi la hijabu katika vituo vya starehe na shule za chekechea ni kukiuka uhuru wa kidini nchini Ufaransa.
Amesema baraza hilo liko tayari kushiriki katika mjadala wa mpango wa marufuku ya hijabu katika Baraza la Seneti la Ufaransa lakini inasikitisha kuwa maseneta wa baraza hilo wamekataa pendekezo la Baraza la Waislamu. Amesema kupasishwa mpango huo ni hujuma dhidi ya wanawake wa Kiislamu na kukanyaga haki zao.
Baraza la Seneti la Ufaransa leo linatazamiwa kuchunguza rasimu ya sheria ya kupiga marufuku vazi la mwanamke wa Kiislamu hijabu katika vituo vya starehe na shule za watoto wadogo.
Jumuiya ya kupambana na kampezi chafu dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa pia imelaani rasimu hiyo na kulitaja swala hilo kuwa ni ubaguzi dhidi ya mama Waislamu ambao wanaandamana na watoto wao kwenye shule za chekechea na vituo vya starehe. 911414

captcha