IQNA

Daktari Muislamu atoa huduma bure za tiba nchini Marekani

17:05 - December 10, 2011
Habari ID: 2236127
Daktari mmoja Muislamu ameanzisha zahanati inayotoa huduma za tiba bure na bila ya malipo kwa watu wenye haja katika jimbo la Carolina kwa lengo la kudhihirisha sura halisi ya Uislamu.
Kituo cha On Islam kimeripoti kuwa Daktari Reshme Khan ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya wanawake ameasisi zahanati hiyo katika mji wa Mount Pleasant kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kiislamu ya Kutoa Misaada ya Kibinadamu Kaskazini mwa Marekani.
Zahanati hiyo ilianza kutoa huduma za tiba bure kwa watu wenye haja mwanzoni mwa mwaka huu na kudhihirisha sura halisi ya dini ya Kiislamu inayotilia mkazo suala la kusaidiwa watu wenye haja.
Hatua hiyo ya daktari Muislamu imekaribishwa na kupongezwa na jamii ya madaktari, viongozi na wafuasi wa dini mbalimbali katika jimbo la Carolina.
Waislamu wamekuwa wakitoa huduma kama hizo za bure za tiba katika maeneo mbalimbali ya Marekani. Mwaka jana kundi moja la madaktari Waislamu lilianzisha zahanati ya Nour katika jimbo la Ohio ambayo inatoa huduma za tiba kwa watu wasiokuwa na bima za tiba na afya.
Vilevile zahanati ya Jumuiya ya Madaktari Waislamu (UMMA) imekuwa ikitoa huduma za bure za tiba kwa muongo mmoja sasa nchini Marekani. Mwaka 1996 kundi moja la wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu vya Marekani pia lilianzisha zahanati ya kwanza inayotoa huduma za bure za tiba nchini Marekani. 912672
captcha