Akizungumza siku ya Ijumaa katika Msikiti wa Imamein Hasanein (as) mjini Beirut, Sayyid Ali Fadhlullah, hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Beirut amesema kuwa Marekani inafanya juhudi za daima za kuzusha na kueneza fitina nchini Lebanon na kwa msingi huo amewataka Walebanon wote kuwa macho na kulinda umoja wao katika kukabiliana na njama na fitina hizo.
Ameitaka serikali ya Lebanon kufanya juhudi zake zote kwa madhumuni ya kuimarisha umoja na mazungumzo ya kitaifa miongoni mwa Walebanon, kutekeleza matakwa yao pamoja na kuboresha viwango vyao vya maisha. Sayyid Ali Fadhlullah amesema wakati umefika wa kuimarishwa uhusiano wa raia na serikali na vilevile hali yao ya kijamii na kimaisha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo Ayatullah Abdul Amir Qabalan, Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon pia alizungumza katika Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika makao makuu ya Baraza hilo na kusema kuwa njia ya mazungumzo ndiyo njia bora zaidi ya kutatua matatizo ya wanadamu badala ya kutumiwa njia za dhulma na ukandamizaji.
Wakati huohuo, Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti wa Mashia nchini Lebanon ameashiria hali ya Syria katika Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Msikiti wa Imam Hassan (as) na kusema kuwa mgogoro wa nchi hiyo inaandaa mazingira ya kuenezwa fitina za nchi za Magharibi katika eneo.
Katika upande wa pili, Sheikh Afif Nablosi, mmoja wa mahakatibu wa Swala ya Ijumaa ya Lebanon amesisitiza katika Kituo cha Sayyida Zahraa (as) mjini Sur kwamba Waislamu wanapasa kuwa macho kuhusiana na matukio ya Plaestina. Amewataka wavunje njama zote za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kutumia vibaya hali ya kulegalega ya nchi za Kiarabu kwa madhumuni ya kuimarisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina. 912612