IQNA

Ikhwani yasema mapinduzi ya nchi za Kiarabu ni ya Kiislamu

13:25 - December 12, 2011
Habari ID: 2237257
Naibu Mwenyekiti wa chama cha Uhuru na Uadilifu tawi la harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri Isam al Aryan amesema kuwa ushindi wa wanaharakati wa Kiislamu katika chaguzi za kwanza huru katika nchi za Misri na Tunisia ni kielelezo kwamba mapinduzi yaliyofanyika katika nchi hizo ni ya Kiislamu.
Al Aryan ambaye alikuwa akihutubia kikao cha chama cha Uhuru na Uadilifu kilichoshinda awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge la Misri, amesisitiza kuwa mwamko wa Kiislamu ndio chachu ya mapinduzi yanayotokea kwenye eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema suala hilo limedhihiri zaidi baada ya ushindi wa vyama vya Kiislamu katika nchi za Misri na Tunisia.
Amesisitiza kuwa nchi ya Libya ina utajiri mkubwa wa mafuta, Sudan ina utajiri wa chakula na Misri inasifika kwa kuwa na nguvu kubwa ya kazi na iwapo nchi za Kiarabu na Kiislamu zinatishirikiana na kusaidiana zinaweza kujitosheleza.
Naibu Mwenyekiti wa chama cha Uhuru na Uadilifu anasema maadui daima wamekua wakifanya njama za kufelisha mapinduzi ya wananchi wa Misri na kwamba harakati ya Ikhwanul Muslimin itafanya juhudi kubwa za kufanikisha mapinduzi hayo.
914070
captcha