IQNA

Isesco yalaani mashambulio ya kigaidi mjini Baghdad

16:05 - December 24, 2011
Habari ID: 2244229
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ISESCO jana Ijumaa lilitoa taarifa likilaani mashambulio yaliyofanywa hivi karibuni na magaidi mjini Baghdad, Iraq.
Taarifa hiyo imeyataja mashambulio hayo yaliyopelekea kuuawa kwa makumi ya watu na kujeruhiwa wengine wengi kuwa ni jinai kubwa dhidi ya binadamu na kuongeza kuwa mauaji hayo yaliyotekelezwa dhidi ya watu wasio na hatia, hayakubaliki kabisa.
Taarifa ya Isesco imesema kwamba mauaji hayo hayatakuwa na natija nyingine ghairi ya kuzua hofu na woga na mivutano kati ya wafuasi wa madhehebu tofauti ya Kiislamu tena katika nchi ambayo inahitajia umoja na mshikamano wa wananchi wake kuliko jambo jingine lolote. Imesema katika kipindi hiki tata, wananchi wa Iraq wanapasa kuzingatia umoja na mshikamano na kujiepusha na masuala yanayowatenganisha katika shughuli zao za kidini na kisiasa ili kuweza kujikwamua kutoka kwenye mgogoro unaowakabili hivi sasa. Imeendelea kusema kuwa Wairaki wanapasa kuimarisha utulivu wa kisiasa nchini na kulinda kujitawala kwa nchi yao kwa kutoruhusu maadui wa kigeni kuingilia masuala yao ya ndani.
Mashambulizi kadhaa ya kigaidi yaliyotokea katika maeneo ya Mashia mjini Baghdad siku ya Alkhamisi yalipelekea watu 68 kupoteza maisha na wengine 183 kujeruhiwa. 921182
captcha