IQNA

Maandamano ya wanazuoni wa al-Azhar kupinga siasa za wanajeshi

16:05 - December 24, 2011
Habari ID: 2244230
Wanazuoni na wanafunzi wa chuo cha kidini cha al-Azhar nchini Misri jana Ijumaa waliandamana katika uwanja wa Tahrir kulaani siasa za ukandamiza za Baraza la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ahram maandamano hayo yaliwashirikisha wanazuoni na wanafunzi wa kiume na kike wa kituo hicho muhimu cha kidini katika ulimwengu wa Kiislamu.
Maandamano hayo yaliyoanza mara tu baada ya kumalizika swala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa al-Azhar, yalimalizikia katika uwanja wa Tahrir katika mji mkuu Cairo. Waandamanaji walipiga nara za kulaani Baraza la Kijeshi na kutaka viongozi wake wakiongozwa na Tantawi wajiuzulu mara moja.
Maandamano hayo ambayo yanahesabiwa kuwa hatua muhimu ya kurejea chuo cha kidini cha al-Azhar katika uwanja wa kisiasa wa Misri, yamefanyika kwa lengo la kulaani hatua ya wanajeshi ya kukandamiza waandamanaji na kuvunjiwa heshima binti mmoja wa Kimisri mbele ya jengo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Wakati huohuo wanamapinduzi na wanawake wa Misri walishiriki katika maandamano makubwa mjini Cairo wakitaka wanajeshi waondoke madarakani mara moja na kuyakabidhi kwa serikali ya kiraia. Vyama na harakati za kimapainduzi ndizo zilizoandaa maandamano hayo. 921236
captcha