Taarifa hiyo imesema kuwa siku hii tukufu ya kuzaliwa Nabii Isa (as) inatoa bishara ya matumaini na wokovu kwa mwanadamu. Imewatakia kheri, fanaka na baraka Walebanon wote na hasa Wakristo wa nchi hiyo kwa mnasaba huu wa kukumbuka uzawa wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.
Hizbullah imeelezea matumaini yake kwamba Mwenyezi Mungu atawabariki Walebanon katika siku hizi za maadhimisho ya uzawa wa Nabii Isa (as) na hivyo kuwawezesha kulinda umoja na mshikamano wao kwa ajili ya kupambana na migogoro mbalimbali ya kieneo na kimataifa. Hizbullah imeendelea kusema kuwa siku ya kuzaliwa Nabii Isa (as) ni fursa nzuri ya kuimarisha juhudi za dini na madhehebu tofauti kwa lengo la kufikia uadilifu na usawa katika jamii. Imesisitiza kuwa hii ni fursa nzuri ya kushirikiana na waliodhulimiwa na wanyonge ambao wanateseka kwa muda mrefu kutokana na ukandamizaji wa madhalimu.
Hizbullah imesisitiza mwishoni mwa taarifa yake kwamba kuendelea kukaliwa kwa mabavu Beit Lahm au kwa jina jingine Bethlehemu, sehemu alikozaliwa Nabii Isa (as) na maeneo mengine matakatifu huko Palestina, kwa ushirikiano wa mabeberu wa dunia na hasa Marekani ni mfano wa wazi wa uchokozi na uvukaji mpaka.
Inasemekana kuwa Nabii Isa (as), mmoja wa Mitume Wakuu wa Mwenyezi Mungu yaani Ulul Azm, alizaliwa huko Beit Laham Palestina tarehe 25 Disemba, miaka 622 kabla ya hijra ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. 922331