IQNA

Kutangazwa mji wa Quds kuwa mji mkuu wa Mayahudi ni ukiukaji wa haki za dini tofauti

14:10 - December 27, 2011
Habari ID: 2246265
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, imetoa taarifa ikikosoa vikali muswada wa kutangazwa mji mtukufu wa Quds kuwa mji mkuu wa Mayahudi na kusisitiza kuwa jambo hilo ni ukiukaji wa wazi wa haki za dini nyinginezo za mbinguni.
Hizbullah imesema kuwa muswada huo ambao unajadiliwa na utawala haramu wa Israel ni hatua nyingine ya kufanywa mji huo mtakatifu kuwa wa Kiayahudi jambo ambalo imesisitiza kuwa ni kughusubiwa na kuporwa haki za dini tofauti na vilevile za taifa la Palestina.
Imesema hatua hiyo ya kibaguzi ya utawala haramu wa Israel ni hujuma na dharau ya wazi kwa Waislamu na Wakristo wote duniani. Imeendelea kusema kuwa huo ni uchokozi wa wazi dhidi ya Waislamu na Wakristo, jambo linalothibitisha kwamba Wazayuni hawaheshimu hata kidogo imani na itikadi za makundi hayo mawili muhimu ya kidini.
Taarifa ya Hizbullah imesema kwamba Wazayuni wamekuwa wakipuuza na kukejeli msimamo wa Waislamu na Wakristo unaosisitiza kwamba mji wa Quds unapasa kuwa kituo muhimu cha kukurubishwa pamoja fikra za wafauasi wa dini zote za mbinguni na kuandaliwa mazingira ya wao kuishi pamoja kwa amani, kuvumiliana na kuheshimiana.
Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo Hizbullah imesema kwamba muswada huo wa Wazayuni umetayarishwa kwa ushirikiano kamili wa taasisi na mashirika ya kimataifa yanayodai kutetea haki za binadamu na kuimarisha usalama na amani duniani, mashirika ambayo yananyamazia kimya tishio la utawala haramu wa Israel si tu kwa usalama wa kieneo pekee bali wa ulimwengu mzima.
Hizbullah imekosoa vikali uzembe na udhaifu mkubwa wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na muswada huo. Imezitaka serikali na mataifa mbalimbali duniani kujitokeza na kusimama mbele ya muswada huo wa kichokozi wa Israel. Imeyataka pia mataifa ya Kiislamu na Kiarabu kufanya juhudi za kukomboa na kutetea mji mtakatifu wa Quds pamoja na utambulisho wake. 923467
captcha