IQNA

Baraza la Waislamu la Ufaransa lawataka wananchi wa nchi hiyo kuimarisha umoja

10:25 - January 02, 2012
Habari ID: 2249594
Baraza la Waislamu la Ufaransa limewataka wananchi wa nchi hiyo kuimarisha zaidi umoja na mfungamano wao pamoja na kuheshimiana.
Kwa mujibu wa tovuti ya atlasinfo, Muhammad Musawi mkuu wa baraza hilo amewatumia Wakristo wa Ufaransa ujumbe wa pongezi na heri ya mwaka mpya wa 2012 na kuelezea matumaini yake kwamba mwaka huu utatoa fursa nzuri kwa wananchi wa nchi hiyo kushirikiana kidini na kuimarisha zaidi urafiki wao.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe huo Musawi amesema kwamba kwa kuzingatia kuwa Ufaransa imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, mwaka huu utatoa fursa kwa Wafaransa kushirikiana zaidi katika kutatua matatizo hayo pamoja na kuwasaidia wenzao wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali.
Amewataka Waislamu wa Ufaransa kusaidia na kuunga mkono juhudi za mashirika na jumuiya za masuala ya kheri za nchi hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Amewataka pia kuchangisha pesa katika mijumuiko ya Waislamu na swala za Ijumaa ili kuwafikishia Waislamu wanaohitajia misaada. Pia ametarajia kuwa vitendo vya chuki vinavyoendeshwa na wasio Waislamu dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu vitapungua na kusimama katika mwaka huu mpya. 927287
captcha