IQNA

Al Azhar yapinga taasisi ya Kiwahabi ya Kuamrisha Mema ya Misri

17:02 - January 07, 2012
Habari ID: 2252704
Kituo cha Kiislamu cha al Azhar kimetangaza kuwa kinapinga Taasisi ya Kuamrisha Mema iliyoanzishwa nchini Misri kwa kuiga Mawahabi wa Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, kuanzishwa kwa chombo hicho kunapingana na uwepo wa al Azhar ambayo ndio marejeo pekee ya kisheria ya kutoa hukumu za kidini nchini Misri.
Gazeti la al Ahram limeripoti kuwa Jumuiya ya Uhakiki wa Kiislamu ya al Azhar imeitisha kikao cha dharura chini ya uongozi wa Sheikh Ahmad Tayyib na kutangaza upinzani wake dhidi ya kuundwa taasisi hiyo ya Kiwahabi.
Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo ya al Azhar imesema kuwa Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar ndio marejeo pekee ya kisheria na kutoa hukumu za kidini nchini Misri na imekuwa ikishughulikia masuala hayo kwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita.
Al Azhar imesema kuanzishwa chombo hicho cha Kiwahabi kunapuuza nafasi ya Kituo cha Kiislamu cha al Azhar na taasisi nyingine za kisheria za Misri na imewataka raia wa nchi hiyo kuwa macho mbele ya jumuiya hiyo ya Kiwahabi. 930345


captcha