Kwa mujibu wa tovuti ya Romandie, Khalid Aliyu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amesema kwamba Waislamu wa Nigeria pia wamehuzunishwa na mashambulio yaliyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya makanisa ya nchi hiyo. Amesisitiza kwamba Waislamu wanalaani vikali kila aina ya shambulio dhidi ya maeneo ya ibada na kuongeza kuwa madai ya Pastor Ayo Oritsejafor wa Jumuiya ya Wakristo ya Nigeria CAN kuwa Waislamu wanafanya juhudi za kufanya mauaji ya umati ya kikabila na kidini dhidi ya Wakristo ni dharau na tishio dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Aliyu amesema matamshi hayo ni sawa na kutolewa hukumu dhidi ya Waislamu kuhusiana na matukio ya hivi karibuni bila kuwepo ushahidi wa kutosha wala kufuatwa misingi ya sheria.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nasru al-Islam amesema kuwa kutolewa matamshi kama hayo ni sawa na kutolewa kibali cha kufanyika vitendo vya ghasia na fujo dhidi ya Waislamu na kuzusha mivutano kati ya jamii mbili hizo muhimu za Nigeria.
Vilevile amewataka Wakristo watambue vyema kwamba sio makanisa ya Wakristo tu ndiyo yanayoshambuliwa na watu wenye itikadi za kupindukia mipaka bali hata Waislamu wenyewe wamekuwa wahanga wa mashambulio hayo katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Amesema badala ya kuchochea ghasia nchini viongozi wa kidini wanapasa kuhubiri umoja na mshikamano kati ya wananchi na kupima maneno yao kabla ya kuyatamka ili kurejesha amani na utulivu unaohitajika.
Jumuiya ya Nasru al-Islam ni muungano wa taasisi na jumuiya nyingine nyingi za Kiislamu za Nigeria. 932383