Katika taarifa hiyo, Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa OIC amelaani kwa maneno makali shambulio hilo lililowalenga waombolezaji na kuua shahidi wengi miongoni mwao na wengine kujeruhiwa.
Ihsanoglu ameyataka makundi yote ya kidini na kisiasa ya Iraq kushirikiana na kujiepusha na hitilafu kwa madhumuni ya kurejesha amani na utulivu wa kudumu nchini humo. Amesema ugaidi unaotekelezwa nchini Iraq una lengo la kuzusha mifarakano baina ya Wairaki na kuhatarisha maslahi ya taifa hilo.
Katibu Mkuu wa OIC ameashiria udharura wa kulindwa amani na usalama wa raia na kusema kuwa jambo hilo linazingatiwa sana na OIC. Amesisitiza kwamba viongozi wa jumuiya hiyo wanashirikiana na viongozi wa Iraq ili kutekeleza Mkataba wa Makka unaosisitiza udharura wa makundi yote ya kidini na kisiasa ya Iraq kushirikiana kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Ihsanoglu ameelezea matumaini yake kwamba viongozi wa nchi hiyo watashirikiana na jumuiya ya OIC katika kuandaa kikao kingine hivi karibuni kitakachojadili njia za kupambana na mielekeo ya kuvuka mipaka na fikra finyu za kidini na kikabila miongoni mwa Wairaki.
Tunakumbusha hapa kuwa mlipuko wa kigaidi uliotokea Basra siku ya Jumamosi tarehe 14 Januari uliua shahidi waombolezaji 53 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 100. Mlipuko huo ulitekelezwa na mwanamke mmoja gaidi aliyekuwa amevalia mavazi ya polisi. 936506