Kwa mujibuwa mwandishi wa IQNA barani Ulaya, maonyesho hayo yalifunguliwa Alkhamisi 26 Januari.
Kwa kutumia nyaraka za kale, filamu, sauti na picha maonyesho hayo yanaangazia historia, safari na uzoefu wa mahujaji wanaosafiri kutoka kila kona ya dunia kuelekea katika Mji Mtakatifu wa Makka.
“Utayarishaji wa maonyesho hayo umekuwa ni somo kubwa kwangu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita”, amesema Qaisra Khan mmoja kati ya wataalamu waliotayarisha maonyesho hayo.
Maonyesho hayo yanaonyesha namna Muislamu anavyoanza kujitayarisha kwa ajili ya Hija ikiwa ni pamoja na kulipa madeni yote na kuwaomba watu msamaha.
Aidha maonyesho hayo yanaonyesha njia ambazo Waislamu wamekuwa wakizitumia kuelekea Makka wakitokea miji kama vile Kufa, Cairo na Damascus. Vilevile wanaoshiriki katika maonyesho hayo wanapewa ufafanuzi kuhusu baadhi ya amali za Hija.
Aghalabu ya athari za kidini katika maonyesho hayo zimetolewa na Nasser Khalili, mmoja kati ya wakusanyaji wakubwa wa sanaa za Kiislamu duniani. ‘Maonyesho haya yana ujumbe wa kidini, kimaanawi, kiibada na kiutamaduni na ni dhihirisho la mligano katika Uislamu’, amesema Khalili. Maonyesho hayo yenye anwani ya ‘Hija: Safari Kuelekea Moyo wa Uislamu’ yataendelea katika Jengo la Makumbusho la Uingereza mjini London hadi Aprili 15.
941585