Katika taarifa hiyo, washiriki wamesema Mwamko wa Kiislamu ni moja ya ahadi za kweli za Mwenyezi Mungu na kwamba karne hii ni karne ya Uislamu.
Washiriki wamesema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini, mhuishaji mkubwa wa Uislamu katika zama hizi, amechangia kwa kina katika harakati za Kiislamu na idiolojia ya Kiislamu duniani.
Aidha vijana Waislamu walioshiriki wamesema hasira na ghadhabu za maadui dhidi ya Uislamu inatokana na Mwamko wa Kiislamu ambao unaashiria nguvu za Uislamu na uwezo wake mkubwa duniani.
Kuhusu kadhia wa Palestina, washiriki wamesema mapambano ya Wapalestina dhidi ya Wazayuni ni suala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Aidha washiriki wameonya kuhusu njama za maadui za kuibua migongano ya kimadhehebu katika umma wa Kiislamu kwa hivyo wametoa wito kwa vijana Waislamu kote duniani kuwa waangalifu na kujiepusha na mifarakano na wazingatie aya ya 46 ya Surat Al-Anfaal isemayo "Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri."
Washiriki vijana katika kongamano hilo la kwanza la aina yake pia wamewaahidi mashahidi Waislamu kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa ulimwengu wa Kiislamu unapiga hatua kubwa za maendeleo na kujitegemea katika uga wa sayansi, utamaduni, siasa, uchumi na sanaa.
Katika kipengee cha mwisho cha taarifa hiyo vijana Waislamu walioshiriki katika Kongamano la siku mbili la 'Mwamko wa Kiislamu na Vijana' wametoa shukrani zao za dhati kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na misimamo yake ya kimantiki na ubunifu wake katika kuutetea na kuuhami Uislamu na Waislamu. Aidha wameishukuru serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuandaa kongamano hilo na kwa ukarimu waliopata.
943977