Huku akiashiria nafasi muhimu ya historia ya Kiislamu ya mji mtakatifu wa Najaf, Katibu Mkuu wa Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu Isesco, amesema kuwa kuarifishwa mji huo kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu katika mwaka huu wa 2012 ni fahari kubwa kwa shirika hilo.
Akifafanua suala hilo, Abdul Aziz bin Othman at-Tuweijri Katibu Mkuu wa Isesco amesema kuwa uamuzi wa kutajwa mji huo mtakatifu kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu ni jambo la kufurahisha mno kwa sababu mji huo umekuwa na nafasi muhimu katika historia ya Kiislamu. Amesema kuchaguliwa mji huo kuwa mji mkuu wa ulimwengu wa Kiislamu kunatokana na nafasi yake muhimu katika kuwaunganisha Waislamu na kuondoa hitilafu zilizopo baina yao.
At-Tuweijri amesisitiza kuwa mji mtakatifu wa Najaf una nafasi muhimu kati ya Waislamu kutokana na kuwepo huko kaburi la Imam Ali (as). Amesema kituo cha elimu ya kidini cha Najaf pia kina nafasi muhimu kati ya Waislamu kwa sababu wanazuoni na maulama mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu wamepata masomo yao katika mji huo, maulama ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu duniani.
Amemaliza kwa kusema kuwa kuwepo fikra na tamaduni tofauti katika mji wa Najaf ni jambo jingine linaloupa mji huo sifa maalumu. 946233