IQNA

Watu wa Gaza wamkaribisha Ban Ki-moon kwa viatu na mawe

16:55 - February 04, 2012
Habari ID: 2267906
Wakazi wa Ukanda wa Gaza wameutupia mawe na viatu msafara wa Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni katika kulalamikia siasa za kibaguzi za umoja huo dhidi ya wananchi wa Palestina.
Hatua ya Ban Ki-moon ya kukataa kuonana na familia za mateka, mashahidi, wamiliki wa mashamba na nyumba zilizoharibiwa na jeshi la utawala haramu wa Israel, wakulima na wagonjwa wa Palestina wakati wa kufanyika safari yake ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza ni jambo lililowakasirisha sana wakazi wa ukanda huo.
Huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa nara tofauti za malalamiko, wakazi hao wamemtaka Ki-moon akomeshe siasa za Umoja wa Mataifa za kuupendelea utawala haramu wa Israel na kumaliza kimya cha umoja huo kuhusiana na mashambulio ya mara kwa mara ya maghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Vilevile Wamemtaka aushinikize utawala huo usimamishe mara moja hatua yake ya kuwateka nyara wabunge na wawakilishi rasmi wa taifa la Palestina. Wakazi wa Gaza wamesema Ban Ki-moon alitangaza rasmi kuwa katika safari yake hiyo hatakutana na kiongozi yeyote wa serikali, jambo linalobainisha wazi siasa za upendeleo za umoja huo kwa utawala ghasibu wa Israel.
Mwaka uliopita pia Bin Ki-moon alichukua hatua kama hiyo ya kukataa kuonana na familia za mateka na mashahidi wa Palestina katika hali ambayo alionana na kuzungumza na familia ya Gilad Shalit, mateka wa jeshi la Israel.946251
captcha