Kwa mujibu wa tovuti ya legyptien, Waziri al-Qausi ameelezea kusikitishwa kwake na matukio machungu ya vifo vilivyotokea siku ya Jumatano katika uwanja wa mpira wa Port Said ambayo yalipelekea kuuawa kwa watu zaidi ya 70. Amesema matukio hayo yalipangwa kwa ajili ya kuvuruga umoja wa Waislamu wa Misri na kwamba hayana natija nyingine ghairi ya kuzusha vurugu nchini.
Amesema dini tukufu ya Kiislamu inakemea na kukataza vikali umwagaji damu ya watu wasio na hatia na kwamba Waislamu wanapasa kuzingatia mafundisho ya Kiislamu na kujiepusha kurudia matukio hayo.
Waziri huyo pia amesema kuwa sherehe zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Maulidi ya Mtume zitasimamishwa kwa muda kutokana na matukio hayo ya kusikitisha.
Siku ya Alkhamisi wizara hiyo iliwaamuru maimamu wa swala za jamaa katika miji yote ya Misri kuzungumzia suala la kuvumiliana na kuishi pamoja kwa amani na vilevile uharamu wa kumwagwa damu ya watu wasio na hatia katika Uislamu katika hotuba zao za Swala ya Ijumaa.
Watu 74 waliuawa katika matukio ya Siku ya Jumatano wakati wa kuchezwa mechi kati ya timu mbili za al-Ahly na al-Masry katika uwanja wa mpira wa Port Said ikiwa ni katika michuano ya ligi ya nchi hiyo. 946587