Kwa mujibu wa tovuti ya Atlasinfo, Wizara ya Habari ya Morocco imechukua hatua ya kupiga marufuku uuzwaji wa toleo la hivi karibuni la jarida la Nouvel Observateur kwa kuchapisha picha zinazoyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, likiwa ni jarida la nne kuchukuliwa hatua kama hiyo ya kisheria na serikali ya Morocco.
Akifafanua suala hilo, Mustafa Khalafi, Waziri wa Habari wa Morocco amesema kuwa serikali imelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya jarida lililotajwa kuchapisha picha hizo za kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu kutoka filamu ya Perspolis ambayo inamdhihirisha Mwenyezi Mungu katika sura ya mwanadamu. Amesema suala hilo halina uhusiano wowote na uhuru wa kujieleza wala kifikra bali linakanyaga moja kwa moja itikadi na matukufu ya Kiislamu.
Filamu hiyo pia iliamsha hasira kubwa ya Waislamu wa Tunisia, baada ya kuonyeshwa nchini humo na baadhi ya watu walio na chuki dhidi ya Uislamu.
Wiki Iliyopita pia serikali ya Morocco ilipiga marufuku jarida jingine la Kikristo la Perelin baada ya kuchapisha picha za kumvunjia heshima Mtume (saw) kinyume na mafundisho ya Kiislamu, jambo lililoamsha hasira ya viongozi wa kidini na kisiasa wa nchi hiyo.
Wizara ya Habari ya Morocco imesema kuwa uchapishaji na uchoraji wa picha zozote zinazohusiana na Mtume na Mwenyezi Mungu ni uvunjiwaji heshima wa moja kwa moja wa matukufu ya Kiislamu na ukiukaji wa kipengee cha 29 cha sheria ya vyombo vya habari ya nchi hiyo.
Magazeti mengine ya Kifaransa yaliyopigwa marufuku hivi karibuni nchini Morocco kutokana na kosa hilohilo ni pamoja na Ghazal na Epress. 947303