IQNA

Wananchi wa Sudan hawana katiba nyingine isipokuwa sheria ya Kiislamu

11:57 - February 05, 2012
Habari ID: 2268666
Jumuiya ya Wanazuoni wa Sudan imetoa taarifa ikitaka kubuniwa kwa kamati maalumu ya kubuni katiba ya kitaifa ya Sudan kwa lengo la kuimarisha misingi ya sheria za Kislamu nchini humo.
Wamesisitiza kwamba wananchi wa Sudan hawaitambui katiba nyingine isiyokuwa sheria ya Kiislamu. Kwa mujibu wa tovuti ya sudaneseonline, wanazuoni hao pia wamesifu hatua ya vyombo vya habari vya Sudan ya kutekeleza shughuli zao kitaalamu, kujiepusha na masuala ya mifarakano na fitina na kuzingatia mafundisho ya Qur'ani katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wamevisifu pia vyama vya kisiasa vya nchi hiyo kwa kuzingatia masuala ya kitaifa na kushirikiana na serikali ya Khartoum. Taarifa ya wanazuoni hao imeyataka makundi yote ya Kiislamu na Kisufi ya nchi hiyo kushirikiana kwa misingi ya takwa na uchaji Mungu.
Kuhusu mapinduzi na mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa katika nchi za Kiarabu, wanazuoni wa Sudan wamesema katika taarifa yao kwamba Uislamu unaonekana wazi katika mapinduzi hayo jambo ambalo wamesisitiza linatoa udharura wa kushikamana zaidi umma wa Kiislamu na mafundisho wa Kiislamu.
Jumuiya ya Wanazuoni wa Sudan pia imesema kuwa ushindi wa vyama vya Kiislamu katika chaguzi zilizofanyika katika nchi za Kiarabu baada ya kutokea mapinduzi ni dalili nyingine inayothibitisha kwamba mwamko unaoshuhudiwa katika eneo ni wa Kiislamu moja kwa moja. 946726
captcha