Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana katika hadhara ya washiriki katika Kongamano la Kimataifa la Mashairi ya Mwamko wa Kiislamu waliokwenda kukutana naye sambamba na siku hizi za kuadhimisha Maulidi ya Mtume Muhammad (saw) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
Mwanzoni mwa kikao hicho kilichotawaliwa na hali ya kimaanawi, hamasa ya mapinduzi yaliyotokea katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na mwamko wa Kiislamu, malenga wa Tusia, Misri, Yemen, Bahrain, Lebanon, Sudan, Iraq, Syria, Saudi Arabia, Kuwait na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walisoma mashairi yao ya kumsifu Mtume Muhammad (saw), mwamko wa Kiislamu, mapinduzi ya wananchi katika eneo hili, Palestina na Quds Tukufu na vilevile kuhusu maadhimisho ya mwaka wa 33 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusimama kidete kwa taifa la Iran.
Baada ya hapo Ayatullah Ali Khamenei alitoa hotuba akizungumzia nafasi na taathira ya mashairi yenye maana za kina na kusisitiza kuwa mashairi ya mwamko wa Kiislamu yanapaswa kutilia maanani malengo makuu ya harakati hiyo kubwa, njia za kufikia malengo hayo aali, maadui na vizuizi vinavyoanzishwa na maadui hao.
Amesema kuwa mashairi hayo ya mwamko wa Kiislamu yanapaswa kusisitiza sana juu ya mchango wa dini, imani juu ya Mwenyezi Mungu na maarifa ya Qur'ani katika harakati ya mwamko wa Kiislamu kwa sababu harakati yoyote inayotegemea itikadi ya kidini hupata kinga na kubakia siku zote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema tukio la mwamko wa Kiislamu lina umuhimu na taathira kubwa kwa mustakbali wa umma mzima wa Kiislamu. Ameongeza kuwa harakati hiyo ni mwamko halisi na wa Kiislamu ambao ni matunda ya ibra nyingi, ufahamu mkubwa na hima ya mataifa ya Kiarabu ya kipindi cha miaka mingi na kwa sababu hiyo si sahihi kuiita harakati hiyo kubwa kwa jina "Msimu wa Machipuo wa Kiarabu".
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa mwamko wa Kiislamu ni harakati isiyo na mwisho ambayo itabadili historia ya Umma wa Kiislamu kwa idhini yake Mwenyezi Mungu.
Amesema harakati hiyo ni kielelezo cha tukio kubwa la kihistoria ambalo litaleta mabadiliko adhimu katika Umma wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa malenga wa Umma wa Kiislamu wanapaswa kuwa na mchango katika tukio kama hilo adhimu.
Akisisitiza juu ya kuzingatiwa umoja na mshikamano wa Kiislamu katika mashairi ya mwamko wa Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amesema njama kubwa zinaendelea kufanywa kwa shabaha ya kuzusha mizozo na mifarakano kati ya Waislamu ili kusambaratisha na kuvunja harakati adhimu ya mwamko wa Kiislamu. Ameutaka Umma wa Kiislamu kushinda vizuizi vyote vya kimadhehebu, kikaumu na kisiasa na kufunga kabisa njia za kuzusha hitilafu kati ya Waislamu.
Ameashiria mchango wa maneno na kalibu katika ustawishaji wa sanaa ya mashairi na akawahimiza malenga wa Umma wa Kiislamu kutilia maanani mambo hayo mawili na kutunga mashairi ya hali ya juu ili mashairi yao yabakie milele na kuwa na taathira kubwa.
Mwanzoni mwa kikao hicho Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu Dakta Ali Akbar Velayati amezungumzia udharura kuwepo mazungumzo na kustawisha zaidi fasihi inayohusu mwamko wa Kiislamu ambayo itazuia kupotoshwa mapinduzi ya wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kumeitishwa Kongamano la Kimataifa la Mashairi ya Mwamko wa Kiislamu ambalo linahudhuriwa na malenga 77 kutoka nchi 10. 948956