Kitabu kikubwa zaidi kuhusu sira, maisha na shakhsia ya Mtume Muhammad (saw) kilichopewa jina la "Huyu Ndiye Muhammad (saw) kilichotayarishwa huko Dubai kinatazamiwa kusajiliwa katika tabu la rekodi za kimataifa la Guinness.
Gazeti la al Sabiil linalochapishwa nchini Jordan limeripoti kuwa mbunifu wa fikra ya kutayarisha kitabu hicho Muhammad Said al Aulaqi amesema kitabu hiki kimeandikwa katika hali ambayo Umma wa Kiislamu unashuhudia kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima Mtume wa Uislamu.
Muhammad Said al Aulaqi ameongeza kuwa kwa sasa kuna haja ya kufanyika juhudi za kuzindua fikra za watu katika ulimwengu wa Kiislamu na kuarifisha shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad kupitia njia ya kuchapisha vitabu vya Kiislamu kama kitabu hiki cha Huyu Ndiye Muhammad (saw).
Amesema kitabu hicho kina uzito wa kilo 1500 na kurasa 420 zenye upana wa mita 4 hadi 5 na kimetayarishwa kwa kipindi cha miezi 9.
Muhammad Said amesema kitabu hicho kitazinduliwa rasmi tarehe 27 Februari. 951884