IQNA

Mashirika ya haki za binadamu yataka mwandishi aliyemvunjia heshima Mtume (saw) aachiliwe huru!

16:21 - February 14, 2012
Habari ID: 2274194
Baadhi ya mashirika ya haki za binadamu ya Magharibi yameanzisha harakati zilizo dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu kwa kutaka Hamza Kashghari mwandishi wa Saudia ambaye hivi karibuni alimvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema aachiliwe huru bila masharti yoyote.
Kwa mujijibu wa CNN moja ya mashirika hayo, Human Rights Watch, limekosoa vikali hatua ya serikali ya Malaysia ya kumkabidhi mwandishi huyo kwa watawala wa Saudi Arabia na kuwataka wamwachilie huru haraka iwezekanavyo, kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kujieleza. Limedai kwamba kwa kumvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) mwandishi huyo eti alikuwa akijaribu tu kujieleza na kuweka wazi imani yake binafsi.
Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika kanda ya Mashariki ya Kati amedai kwamba Malaysia imevunja sheria kwa kumkabidhi Kashghari kwa watawala wa Saudia na kwamba watawala hao pia wamepuuza sheria kwa kumtia mbaroni mwandishi huyo kutokana na itikadi zake.
Ameendelea kudai kwamba mwandishi huyo hatahukumiwa kiuadilifu nchini Saudia kwa sababu baadhi ya wanazuoni wa nchi hiyo tayari wametoa fatuwa za kuritadi na kunyongwa dhidi yake.
Umoja wa Ulaya pia umelaani kitendo cha Malaysia kumkabidhi mwandishi huyo kwa watawala wa Saudia na kuongeza kuwa Malaysia ilipasa kuzingatia kile ulichokitaja kuwa sheria za kimataifa na kutomkabidhi mwandishi huyo kwa Saudi Arabia.
Kashghari amemvunjia heshima Mtume Mtukufu kupitia mitandao ya kijamii ukiwemo wa Twitter. Hata hivyo amenukuliwa akisema kuwa amejuta kutokana na kitendo hicho na eti kumtaka Mwenyezi Mungu amsamehe. 953290
captcha