Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa jana mjini Tehran amesema kuwa, kuhudhuria kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi ujao wa duru ya tisa ya Bunge la Iran kutakuwa jibu kwa vitisho vya hivi karibuni vya maadui wa taifa hili.
Ayatullah Muhammad Imami Kashani amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Sala ya Ijumaa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran. Amesisitiza kwamba, adui ameingiwa na kiwewe na sasa anapanga njama za kuwafanya wananchi wa Iran wasihudhurie kwa wingi katika uchaguzi ujao wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge la Iran.
Ayatullah Kashani ameashiria njama za maadui za kuushinikiza Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kwamba, hitajio la Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi hiki ni umoja na mshikamano.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria vikwazo vya maadui katika uga wa nishati ya mafuta na benki vya nchi za Ulaya na kusisitiza kwamba, licha ya kuweko vikwazo hivyo gurudumu la maendeleo hapa nchini linaendelea kwa kasi kubwa.
954835