Nargis bin Abidah mwanachama wa kamati ya kupinga Uzayuni ya Collectif Chalon Palestine ya Ufaransa amemwabia mwandishi wa IQNA kuwa kuchochea chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu ni njia inayotumiwa kupotosha fikra za waliowengi duniani. Ameashiria vitendo kama vile kuongezeka hujuma dhidi ya misikiti barani Ulaya na Wazayuni kuvamia Msikiti wa Al Aqsa kuwa vitendo vinavyofanyika kwa malengo hayo.
Wakati huo huo ,sambamba na kuongezeka wimbi la malalamiko ya Waislamu kote duniani dhidi ya kitendo cha askari wa Marekani cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu nchini Afghanistan, maudhui hiyo sasa imekuwa mjadala mkubwa katika kampeni za uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Wanaowania urais kwa tiketi ya chama cha Republican wamemkosoa waziwazi Rais Barack Obama wa Marekani na wamemlaumu kwa kuelezea masikitiko yake kuhusu kitendo cha askari wa nchi hiyo cha kuchoma moto Qur'ani huko Afghanistan.
Mitt Romney na Rick Santorum ambao wanachuana kukiwakilisha chama cha Republican katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani wamemkosoa Obama kwa kueleza kwamba amesikitishwa na kitendo cha askari wa nchi hiyo cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu. Rick Santorum amesema hakuna jambo lililotokea linalolazimu kuomba radhi.
Kwa sasa uhusiano wa Marekani na Afghanistan umekumbwa na matatizo baada ya askari wa serikali ya Washington kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu. Katika siku chache zilizopita viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali ya Washington wamejaribu kutuliza hasira za Waafghani na Waislamu kote duniani kwa kulaani kitendo hicho cha askari wa Marekani huko Afghanistan na kuunda tume ya kuchumguza tukio hilo. Hata hivyo mashambulizi yanayofanywa dhidi ya askari wa Marekani huko Afghanistan ni ishara kwamba taathira mbaya za tukio hilo la kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu haziwezi kumalizwa kwa maneno matupu.
Wakati huo huo makundi yenye misimamo mikali na inayopendelea vita katika pande zote mbili yaani huko Marekani na Afghanistan yanafanya juhudi za kutumia malalamiko hayo ya Waislamu kama kisingizio kipya cha kuchochea mapigano na machafuko zaidi. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kumeshuhudiwa mara kwa mara kwamba makundi yanayopendelea mapigano na utumiaji wa mabavu katika baadhi ya nchi za Kiislamu yamekuwa yakitumiwa na Wamagharibi kama nyenzo za mauaji ya kigaidi na hivyo kutayarisha mazingira ya uingiliaji wa nchi za Magharibi katika masuala ya nchi za Kiislamu. Inaonekana kuwa hali hii pia imeanza kujitokeza katika kadhia ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Afghanistan.
Hatua au kitendo chochote cha kuvunjia heshima itikadi na matukufu ya kidini ni jambo ambalo halikubaliwi kwa hali yoyote. Pamoja na hayo watu wanaowania madaraka na kiti cha urais huko Marekani wanakieleza kitendo kiovu cha kuvunjiwa heshima na kuchomwa moto kitabu kitakatifu cha Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu kuwa ni jambo lisilokuwa na umuhimu.
Ni kweli kwamba Rick Santorum, Mitt Romney na Newt Gingrich wametoa matamshi hayo katika kampeni zao za kutaka kumwangusha Barack Obama, lakini pia tunapaswa kuelewa kwamba, misimamo kama hiyo ina asili na misingi ya kiitikadi ya mrengo wenye siasa za kufurutu mipaka nchini Marekani ambao unapuuza na kudharau thamani za kidini za watu wengine. Mrengo huu unakiona hata kitendo cha kuomba radhi tu kwa maneno matupu kuwa ni dhambi kubwa!
961981