IQNA

Kiongozi Muadhamu: Wananchi wa Iran watatoa pigo jingine kubwa kwa maadui

11:46 - March 01, 2012
Habari ID: 2283600
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Jumatano hii ameonana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali pamoja na familia za mashahidi na watu wanaojitolea katika njia ya haki na kusisitiza kwamba, uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran unaotarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii una umuhimu mkubwa zaidi ikilinganishwa na chaguzi za huko nyuma.
Aidha ameashiria umuhimu mkubwa wa kujitokeza kwa wingi sana wananchi katika uchaguzi huo wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa taifa la Iran litatoa pigo jingine kubwa zaidi kuliko lile walilolitoa Bahaman 22 (Februari 11 wakati wananchi wa Iran walipojitokeza kwa mamilioni katika maadhimisho ya miaka 33 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran) na watawathibitishia kivitendo azma na irada yao isiyotetereka na kuifanya kambi ya kibeberu ishindwe kufanya lolote mbele ya taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia propaganda kubwa na za kila upande za miezi kadhaa sasa za vyombo vya habari vya kibeberu vinavyofanya njama za kuwazuia wananchi wa Iran wasishiriki kwenye uchaguzi huo wa bunge na kuongeza kuwa, sehemu yoyote ile duniani, uchaguzi unaowashirikisha watu wengi unahesabiwa kuwa ni uchaguzi uliofana na unaonesha kuwa macho wananchi na kuukubali kwao mfumo wao wa utawala.
Ameashiria pia asimilia ndogo ya wananchi wa Marekani wanaoshiriki kwenye chaguzi mbali mbali za Rais katika miaka ya hivi karibuni na kukumbusha kuwa, asilimia ya watu wanaojitokeza katika uchaguzi wa Rais nchini Marekani haiwezi kufananishwa hata kidogo na idadi kubwa ya watu walioshiriki kwenye uchaguzi wa Rais wa mwaka 2009 nchini Iran na uchaguzi wa Bunge la Nane la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba lengo la propaganda kubwa za vyombo vya habari vya kibeberu ni kutaka kuwazuia wananchi wa Iran wasijitokeza kwa wingi katika chaguzi za nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kitu ambacho yeye kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu anakihisi na kukipa uwezekano mkubwa wa kutokea ni kwamba taifa la Iran litatoa pigo kubwa zaidi kwa mabeberu katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, nyoyo za Mwenyezi Mungu na uongofu wao uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na madhali nyoyo za wananchi, viongozi na watu wenye uchungu zitaendelea kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Naye atawafungulia njia na kuwapa taufiki Yake na Inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu taufiki hiyo wataipata tena wananchi wa Iran katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa.
Amesisitiza kuwa, kushiriki kwa wingi katika uchaguzi kwa kweli litakuwa ni pigo kubwa sana kwa mabeberu na ameongeza kuwa, jambo lililo muhimu zaidi katika uchaguzi ni kushiriki kwa wingi wananchi kwani kadiri wananchi watakavyoshiriki kwa wingi mkubwa ndivyo itakapowezekana kuunda bunge lenye nguvu na la watu wenye mashujaa zaidi na kwamba bunge la namna hiyo ndilo litakaloweza kufikisha kwa njia nzuri zaidi sauti ya wananchi wa Iran kwa walimwengu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, sambamba na kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo, suala la kuchagua watu bora zaidi wa kuwapeleka bungeni nalo ni jambo muhimu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kwamba, umuhimu na unyeti wa uchaguzi wa siku ya Ijumaa ni mkubwa zaidi kuliko chaguzi za huko nyuma na kusisitiza kwamba, umuhimu na unyeti wa uchaguzi huo unatokana na kwamba kambi ya kibeberu imeshatumia silaha zake zote dhidi ya taifa la Iran, na hivi sasa imebakiwa na silaha yake ya mwisho, hivyo wananchi wanapaswa kusimama imara na kuwaonesha maadui irada na azma yao thabiti ili kambi ya kibeberu itambue kuwa, haiwezi kukabiliana hata kidogo na taifa hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi wanayotoa waziwazi na hadharani viongozi wa kambi ya kibeberu kuhusiana na malengo yao ya kuiwekea mashinikizo na vikwazo Iran wakisema kuwa ni kuwakatisha tamaa wananchi wa taifa hili na kuongeza kuwa, Marekani, Magharibi na Uzayuni wanafanya njama za kuwazuia wananchi wa Iran wasiendelee na harakati yao katika njia iliyopelekea kuamka watu katika ulimwengu wa Kiislamu na taifa hili kuwa kigezo kizuri kwa mataifa mingine na maadui hao wanataka kuwaonesha watu wa mataifa mengine kwamba taifa la Iran lililoko mstari wa mbele katika njia hiyo limevunjika moyo na limeshakata tamaa na wanajaribu kuonesha kwamba kigezo hiki kimefeli.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, jambo la ajabu ni kuwa baada ya kupita zaidi ya miaka 30 ya tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, taifa la nchi hii hivi sasa limekuwa kakamavu zaidi, hai zaidi, imara zaidi na lenye nia ya kweli kabisa ya kuendelea na njia yake licha ya kuongezeka mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi, kipropaganda na kiusalama dhidi ya taifa hili.
Ametanabahisha kuwa, maandamano ya Bahman 22 (Februari 11) mwaka huu pamoja na harakati adhimu ya wananchi katika kuunga mkono mfumo wa Kiislamu nchini Iran ni pigo kubwa kwa mabeberu kwani maadui wa taifa la Iran wana hamu kubwa ya kuingiza barabarani vijikundi vya vibaraka wao (ili vifanye maandamano) dhidi ya taifa la Iran (lakini wameshindwa).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia maandamano ya wananchi wa nchi za Ulaya dhidi ya tawala za nchi hizo na kuongeza kuwa, ile ndoto ambayo adui alikuwa anaiota kutokea nchini Iran, imemgeukia mwenyewe na huu ni ushindi kwa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, taifa la Iran licha ya kuweko mashinikizo makubwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kuuliwa shahidi wasomi na wataalamu wake vijana, kamwe halijawahi kuruhusu njama za maadui zifanikishe malengo yake dhidi ya taifa hili.
Aidha ametoa tathmini jumla kuhusu hali ilivyo nchini Iran hivi sasa na kuongeza kuwa, unapoiangalia hali hiyo kwa mtazamo wa kiistratijia utaona kuwa leo hii taifa la Iran linaendelea na harakati yake ya kupiga hatua mbele za kimaendeleo katika vipengee na nyanja zote na hivi sasa liko imara zaidi na lina nia madhubuti zaidi ya kufanikisha malengo yake kuliko wakati mwingine wowote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia ukakamavu na nishati waliyo nayo vijana wa Iran na kuongeza kuwa, mashahidi ambao wengi wao ni katika kizazi cha vijana leo hii wamekuwa ni kigezo kikubwa na muhimu sana kwa vijana wenzao na kwa matabaka yote mengine ya wananchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mifano ya vijana waliokuwa vigezo vizuri katika historia ya Uislamu hususan Imam Hassan Askari AS na Imam Jawad AS na kuongeza kuwa, mashahidi ambao ni kigezo cha vijana na matabaka mengine ya wananchi, wanaangalia hatima na kazi za taifa la Iran na kwamba hatua yoyote na kujitokeza kwa namna yoyote ile wananchi kwa ajili ya kuongeza kasi ya harakati hii ya taifa la Iran na kuipeleka mbele nchi bila ya shaka yoyote huifurahisha roho ya Imam wetu mtukufu na roho za mashahidi.
962970
captcha