IQNA

Kiongozi Muadhamu aagiza kuundwa Baraza Kuu la Mawasiliano ya Mtandao wa Kompyuta

10:39 - March 08, 2012
Habari ID: 2287833
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameagiza kuundwa Baraza Kuu la Mawasiliano ya Mtandao wa Kompyuta chini ya uongozi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran na kuainishwa wajumbe wa kisheria na wataalamu wa baraza hilo.
Ayatullah Khamenei ameashiria taathira kubwa za kanali ya kimataifa ya intaneti katika maisha ya mwanadamu na jamii kwa ujumla na kueleza kuwa, kuna udharura wa kuwekwa mipango mizuri kwa lengo la kuzuia maafa yanayotokana na Intaneti na pia kustafidi na fursa inayopatikana kupitia mtandao huo kwa ajili ya kutoa huduma bora na kubwa kwa jamii.
Amesema hilo ni moja ya sababu zilizopelekea kuundwa Baraza Kuu la Mawasiliano ya Mtandao wa Kompyuta nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, baraza hilo lina jukumu la kuasisi kituo kitakachojulikana kwa jina la "Kituo cha Taifa cha Mawasiliano ya Mtandao wa Kompyuta." Ayatullahil udhmaa Ali Khamenei amesema, anataraji kuwa juhudi kubwa zitafanywa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kituo hicho na kwamba vyombo vyote nchini vina jukumu la kutoa mashirikiano ya pande zote kwa kituo hicho.
Baraza hilo litakaloongozwa na Rais Ahmadinejad litawajumuisha pia maafisa wa ngazi ya juu kama vile Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama, Mkuu wa Shirika la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), na Mawaziri wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano, Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu na wa Usalama wa Taifa.
967513
captcha