Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Arab News, wiki ijayo Saleh anakusudia kuondoka nchini humo na kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na hatimaye kuelekea mji mkuu wa Russia, Moscow.
Baadhi ya duru zinasema atabakia Moscow hadi hapo hali ya ukosefu wa amani na maandamano vitakapopungua sambamba na mrithi wake Abdurabuh Mansur Hadi kuidhibiti nchi hiyo kikamilifu. Imearifiwa kuwa serikali ya Russia imesema iko tayari kumpa Swaleh hifadhi ya daima.
Gazeti la Al Akhbar al Youm limeandika kuwa Imarati imekataa kumpa dikteta Saleh hifadhi ya kisiasa.
Wakati huo huo dikteta huyo wa Yemen Ali Abdallah Saleh amekubali kung'atuka katika cheo cha ukuu wa chama cha Kongresi ya Wananchi nchini Yemen.
Waledi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea kuwepo nchini Yemen dikteta huyo, ni moja ya sababu zinazozuia kutekelezwa mpango wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.
Licha ya kupita mwaka mmoja wa mwamko wa Kiislamu na harakati za mapinduzi ya Wayemen yaliyomng'oa madarakani dikteta Abdallah Saleh, lakini bado watu wa karibu wa dikteta huyo wangali wanaongoza na kushikilia nyadhifa muhimu katika utawala wa hivi sasa wa nchi hiyo. Jambo hilo limewakasirisha sana Wayemen ambao wanaamini kwamba baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zinashirikiana kwa karibu na Marekani kwa lengo la kuvuruga harakati na mapinduzi yao.
996873