Kwa mujibu wa gazeti la an-Nahar al-Jadid linalochapishwa huko Algeria mashirika mawili hayo ya kutetea haki za binadamu yameitaka serikali ya Imarati iwaachilie huru wanaharakati hao tisa wa Kiislamu wanaofungamana na kundi la Ikhwanul Muslimin.
Huku yakiitaka serikali hiyo iache kuwakamata ovyo watu wanaolalamikia masuala tofauti nchini humo, mashirika hayo yamesema kwamba watu hao waliotiwa nguvuni na serikali ya Imarati walikuwa wakitetea haki yao ya kimsingi ya kujieleza na wala hawakuchochea vitendo vyovyote vya ghasia.
Mashirika hayo pia yametaka utawala wa Imarati uwaachilie mara moja wanaharakati wengine 6 wa Kiislamu waliotiwa nguvuni nchini humo mwishoni mwa mwaka uliopita kwa tuhuma za eti kushirikiana na mashirika ya kigaidi.
Watawala wa Imarati wamekuwa wakikabiliana kwa mabavu na ukandamizaji na kila sauti inayotetea uhuru na uadilifu nchini humo hata kama itatoka kwa watu wao wa karibu kama vile Sheikh Sultan bin Kaid al-Qassimi ambaye anazuiliwa jela kwa kutetea misingi ya uhuru wa kujieleza katika ufalme huo. 997344