Kasisi Scott Morgan wa kanisa la United Church of Christ katika jimbo la Virginia nchini Marekani, ameanza kutoa mafunzo na tafsiri za Qur'ani katika kanisani ikiwa ni jibu lake dhidi ya kitendo cha Kasisi Terry Jones wa jimbo la Florida cha kukivunjia heshima kitabu hicho kitakatifu kwa kukichoma moto.
Kasisi Morgan amekuwa akitoa maelezo na tafsiri kuhusiana na aya za Qur'ani zinazozungumzia haki za wanawake, amani, upendo na kuishi pamoja kwa amani Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo. Kwa kutoa maelezo hayo pamoja na mifano ya maisha ya Mtume Mtukufu (saw), kasisi huyo anakusudia kuonyesha kwamba Uislamu unapinga vikali kutumiwa vitendo vya nguvu na mabavu dhidi ya wasiokuwa Waislamu na kusisitiza juu ya umuhimu wa nafasi ya wanawake wa Kiislamu katika jamii.
Kasisi Morgan anasema amechagua kuzungumzia masuala mawili muhimu ya utumiaji nguvu na haki za wanawake kwa sababu yanafuatiliwa kwa hisia maalumu nchini Marekani. Anasema atakuwa amefanikiwa kwa kiwango kikubwa iwapo juhudi zake hizo zitapelekea hata idadi ndogo tu ya Wamarekani kufahamu ukweli na kutambua uongo unaoenezwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo kuhusiana na dini ya Kiislamu.
Televisheni moja ya Marekani imeakisi masomo ya tafsiri ya Qur'ani yanayotolewa na Kasisi Morgan na kusema kuwa hatua yake hiyo ni nzuri na ya kuvutia hasa katika kipindi hiki ambapo Kasisi Terry Jones amevunjia heshima kitabu hicho cha mbinguni kwa kukichoma moto. 1002994