Wakati huo huo , mwalimu mmoja wa chuo kikuu nchini Lebanon amefichua kuwa, mateka na wafungwa wengi walioko katika jela za kutisha za utawala wa Israel wanapata mateso makali.
Muhsin Saleh ambaye ni mwalimu katika chuo kikuu cha Lebanon aliyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya Press TV na kusema kuwa, mateso wanayoyapata mateka wa Kipalestina katika jela za kutisha za utawala wa Kizayuni, yanapingana kabisa na sheria za kimataifa za haki za binaadamu. Amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa vielelezo vya takwimu asilimia 90 ya mateka na wafungwa wa Kipalestina waliomo katika jela hizo za utawala wa Israel wanapata mateso makali kutoka kwa vikosi vya utawala huo.
Katika upande mwingine Naibu Waziri wa Masuala ya Mateka na Wapalestina Walioachiliwa Huru wa serikali ya Palestina amezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kuwaunga mkono zaidi mateka wa Kipalestina na kuhakikisha wanatolewa katika jela za kutisha za utawala wa Kizayuni.
Muhammad al Katri amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Alam akiweko mjini Ghaza na kuongeza kuwa, mateka wa Kipalestina wanakabiliwa na hali mbaya sana katika jela za Israel.
Amesema, mateka wa Kipalestina wanakabiliwa na hali mbaya mno hivi sasa wakiwa katika wiki ya nne ya kususia chakula na kadiri siku zinavyopita, ndivyo hali ya Wapalestina hao inavyozidi kuwa mbaya.
Hata hivyo amesema, msimamo wa mateka hao ni imara na wanakabiliana vilivyo na ukandamizaji wanaofanyiwa na askari magereza wa Israel.
Naibu Waziri huyo wa serikali ya Palestina ameongeza kuwa, ana matumaini harakati zinazofanyika huko Palestina na katika nchi za Kiarabu na Kiislamu za kuwaunga mkono mateka hao, zitaongezeka, kwani mateka hao wanapigania haki zao za kimsingi ikiwa ni pamoja na kuikomboa Palestina kutoka katika makucha ya Wazayuni.
1006883