IQNA

Husni Mubarak ahukumiwa kifungo cha maisha jela

14:59 - June 02, 2012
Habari ID: 2339358
Dikteta wa zamani wa Misri Husni Mubarak amehukumiwa kifungo cha maisha jela kutokana na mauaji yaliyotekelezwa wakati akiwa rais katika siku za mwamko wa Kiislamu mapinduzi yaliyojiri nchini humo Februari 11.
Katika hukumu iliyotolewa na mahakama moja huko Cairo, dikteta huyo wa zamani pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Habib al Adli walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kuwaua karibu waandamanaji 900 katika siku za kuanza mwamko wa Kiislamu nchini humo.
Hukumu hiyo imepelekea kuibuka makabiliano nje ya mahakama baina ya familia za mashahidi 900 waliouawa na vikosi vya usalama. Wananchi waliokuwa na hasira wameitaja mahakama hiyo kuwa haramu huku wakitaka dikteta wa zamani Mubarak ahukumiwe kifo.
Hukumu hiyo inakuja huku Wamisri wakitarajiwa kuchagua mmoja kati ya mgombea wa Ikwanul Muslimin Mohammad Morsi na Waziri Mkuu wa Zamani wa utawala wa Mubarak Ahmad Shafiq Juni 16 na 17.
Kwingineko Baraza Kuu la Kijeshi la Misri limetangaza kwamba hali ya hatari nchini humo imemalizika, ikiwa ni baada ya kupita miongo mitatu tangu kutangazwa sheria hiyo na dikteta Husni Mubarak. Baraza hilo limetoa taarifa na kutangaza kumalizika hali hiyo ya hatari iliyotangazwa nchini humo mwaka 1981, baada ya kuuawa rais wa zamani wa nchi hiyo Anwar Sadat.
Sheria hiyo iliwapa ruhusa maafisa wa usalama wa Misri kuvunja kwa kiasi kikubwa haki za msingi za wananchi kukiwemo kuwatia mbaroni watu kiholela na bila sababu zozote, na pia kubanwa uhuru wa vyombo vya habari.
Wakati huo huo katika siku ya kwanza ya kuondolewa hali ya hatari nchini Misri wananchi wa nchi hiyo jana Ijumaa kwa mara nyingine walifanya maandamano na kukusanyika katika Meidani ya Tahrir mjini Cairo. Maandamano hayo yaliitishwa na taasisi na jumuiya mbalimbali za kisiasa na kimapinduzi za Misri, kwa lengo la kutetea na kulinda mapinduzi ya wananchi. Wataalamu wa mambo wanasema, kukosekana kiongozi mmoja mwenye itibari katika mapinduzi ya Misri kulisababisha wananchi kutoshirikia kwa kiasi kikubwa zaidi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo, jambo ambalo limempelekea Ahmad Shafiq ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Husni Mubarak kuingia katika duru ya pili. Wakati huo huo hivi sasa kuna wasiwasi kuhusiana na kurejea tena madarakani mabaki ya utawala wa Mubarak, kupoteza utambulisho na kuporwa mapinduzi ya Misri. Hii ndiyo sababu, sambamba na kuhitimishwa hali ya hatari nchini humo, wananchi wa Misri jana walimiminika kwa mara nyingine mabarabarani ili kulinda mapinduzi hayo.
1022284
captcha