IQNA

Wanazuoni wa Lebanon walaani mlipuko wa kigaidi karibu na Haram ya Bibi Zainab (as) nchini Syria

19:17 - June 16, 2012
Habari ID: 2347950
Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu ya Lebanon imetoa taarifa ikilaani shambulio lililofanywa siku ya Alkhamisi na magaidi karibu na Haram ya Bibi Zainab (as) mjini Damascus nchini Syria.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Intiqad linalochapishwa Lebanon, jumuiya hiyo imesema kwamba makundi ya kigaidi yanayofungamana na madola ya kibeberu ya Magharibi yanafanya kila jinai kwa lengo la kuvuruga amani na uthabiti wa Syria. Imesema baada ya madola hayo kushindwa kuwachochea wananchi wa Syria wasimame dhidi ya serikali yao sasa yanatumia ugaidi na jinai kuigawa nchi hiyo katika maeneo tofauti.
Imesema kulengwa Mashia huko Halab nchini Syria na kulipuliwa kwa bomu basi moja lililokuwa limewabeba wafanyaziara huko Iraq si jambo lililotokea hivihivi bila mpangilio maalumu, bali ni jambo lililopangwa vyema kwa lengo la kuchochea ghasia na machafuko ya kimadhehebu kati ya Masuni na Mashia wa nchi hizo na vilevile nchini Lebanon. 1030638
captcha