IQNA

Vikosi vya Israel vimeua Wapalestina, 2,300 Ghaza

17:02 - June 19, 2012
Habari ID: 2349795
Vikosi vya utawala haramu wa Israel vimewaua shahidi Wapalestina 2,300 na kuwajeruhi wengine 7,700 katika Ukanda wa Ghaza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imetangaza Idara ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu UNOCHA.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, shirika hilo la Umoja wa Mataifa katika ripoti kuhusu mzingiro wa Israel huko Ghaza limesema asilimia 27 ya waliouawa Ghaza ni wanawake na watoto.
Mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani huko Ghaza uliingia mwaka wake wa sita Alkhamisi iliyopita. Katika mzingiro huo unaotekelezwa na utawala haramu wa Israel, Wapalestina huko Ghaza hawana idhini ya kuingiza bidhaa muhimu na za dharura kama vile madawa, chakula na vifaa vya ujenzi.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema mzingiro wa Israel umevuruga maisha ya wavuvi 35,000 Wapalestina huku Wakulima wakipoteza mazao ya tani 75,000 kila mwaka kutokana na vizingiti vinavyowekwa na Israel mipakani.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa hatua ya Israel ya kulizingira eneo la Ukanda wa Ghaza ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, hatua ambayo imewasababishia matatizo mengi raia wa Palestina wa eneo hilo. Jopo la wataalamu watano wa haki za binadamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa lililowasilisha taarifa yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la umoja Septemba mwaka 2011 lilieleza huko Geneva Uswisi kuwa, mzingiro wa kiuchumi wa utawala wa Kizayuni huko Ghaza umewaadhbu pakubwa raia wa Kipalestina wa eneo hilo, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Wapalestina wamekuwa chini ya mzingiro wa Wazayuni tokea mwaka 2007 na kosa lao kubwa kwa mujibu wa Wazayuni ni kuwa walishiriki katika uchaguzi huru wa kidemokrasia na kumchagua Ismail Haniya wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kuwa kiongozi wa serikali yao.
1033084
captcha