IQNA

Maadhimisho ya kuzaliwa Imam Mahdi (af) yafanyika Nigeria

16:57 - July 07, 2012
Habari ID: 2362661
Maadhimiho ya kuzaliwa Imam Mahdi (af) yalifanyika siku ya Alkhamisi Julai Tano huko katika mji wa Kaduna nchini Nigeria kwa ushirikiano wa Taasisi ya Thaqalain.
Adama Adam, mhadhiri wa chuo kikuu ambaye alizungumza katika maadhimisho hayo alisema kuwa Waislamu wanaosubiri kudhihiri kwa Imam Mahdi (af) wanapasa kuzingatia takwa na kumwomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwa mtukufu huyo.
Sheikh Hamza Muhammad aliyekuwa mzungumzaji wa pili mara tu baada ya kumalizika ufunguzi wa maadhimisho hayo kwa kisomo cha Qur'ani, alizungumzia Imam huyo aliyeahidiwa kudhihiri mwishoni mwa zama katika mtazamo wa dini zisizo za Kiislamu. Amesema fikra ya umahdawi haipatikani tu katika mafundisho ya Kiislamu bali katika dini zote za mbinguni ambapo zinagusia suala la kudhihiri mwokozi katika siku za mwisho za uhai wa mwanadamu humu duniani, ambaye ataeneza uadilifu na kuwaokoa wanadamu wanaokandamizwa na madhalimu.
Sheikh Muhammad amesema mwishoni mwa hutuba yake kwamba Mtume Mtukufu (saw) aliahidi kwamba maimamu watakaowaongoza Waislamu baada ya kuondoka yeye ni 12 na kwamba wa mwisho miongoni mwao atakuwa Imam Mahdi (af).
Mbali na maadhimisho hayo sherehe zingine za maadhimisho hayo zilifanyika katika Husseiniya ya Baqiyatullah, kwa udhamini wa Sheikh Ibrahim Ya'qub Zakzaki, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Maelfu ya wafuasi na wapenzi wa Imam Mahdi (af) kutoka kila pembe za Nigeria walihudhuria sherehe hizo wangine wakifika huko kwa miguu. 1046417
captcha