Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha uzawa wa Imam Mahdi (af) zilizofanyika katika Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Jakarta Indonesia, Hassan Rahimpour Azghadi mwanachama wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran ametolea mitazamo ya wanazuoni mashuhuri wa Kisuni na kusisitiza kuwa suala na Imam Mahdi ni jambo la msingi ambalo limeenea miongoni mwa wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu. Amesema kupigania uadilifu, kujiepusha na maisha ya kifahari kupindukia, kupigana na utaghuti na dhulma, kujali wananchi na kuzingatia maadili pamoja na ukamilifu ni miongoni mwa sifa muhimu zinazopasa kuzingatiwa na Waislamu katika kipindi cha gheiba ya Imam Mahdi (af).
Msomi huyo amesisitiza kwamba wanaosubiri kudhihiri kwa mtukufu huyo wanapasa kuwa na sifa hizo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuhudumia serikali ya kimataifa ya mtukufu huyo atakapodhihiri tena humu duniani.
Sherehe nyingine kama hizo zilifanyika katika maeneo tofauti ya Jakarta ambapo wazungumzaji waligusia maisha na sifa za Imam Mahdi na kukumbusha kwamba atakapodhihiri ataleta na kueneza uadilifu na usawa katika pembe zote za dunia baada ya kutawaliwa na dhulma na uonevu.
Miongoni mwa sherehe hizo za kuadhimisha uzawa wa Imam Mahdi (af) mjini Jakarta ni zile zilizoandaliwa na Taasisi ya al-Muntadhar na Aalil Bait (as).1050434