Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika mkutano huo kuwa nafasi ya mwakamke katika harakati adhimu ya mwamko wa Kiislamu haina mbadala na huku akiashiria uzoefu wenye baraka nyingi sana wa wanawake wa Kiislamu katika ushindi na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, bila ya shaka yoyote kama uwepo wa wanawake utaendelea kuwepo kwa nguvu na kwa upana katika harakati iliyobarikiwa ya mwamko wa Kiislamu, basi bila ya shaka yoyote mataifa ya Kiislamu yataendelea kushuhudia ushindi mwingi mkubwa katika siku za usoni.
Amesema, kukusanyika pamoja wanawake bingwa wa Kiislamu kutoka nchi 85 tofauti za dunia kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Mwamko wa Kiislamu ni fursa muhimu mno ya kuweza kuelewana zaidi akinamama wa ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Maelewano na mafahamiano yaliyopatikana katika mkutano huo ni utangulizi wa kuweza kuanzishwa harakati yenye taathira kubwa zaidi na ya kudumu katika juhudi za kuhuisha utambulisho na shahkhsia ya wanawake wa Kiislamu duniani.
Kiongozi Muahdamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia njama za miaka 100 ambazo ni njama tata na za pande zote za madola ya Magharibi za kujaribu kuwapotosha wanawake wa Kiislamu na kuwaweka mbali na utambulisho wao wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Jitihada za akinamama wenye vipaji katika ulimwengu wa Kiislamu za kuhuisha utambulisho huo, ni utumishi mkubwa sana kwa umma wa Kiislamu kwani kuthamini utambulisho wao, kuwa macho na kuwa na muono mpana na wa mbali wanawake wa Kiislamu kutakuwa na taathira kubwa sana kwa harakati ya mwamko wa Kiislamu na katika heshima na utukufu wa umma wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mtazamo wa Magharibi kuhusu "mwanamke" kuwa ni mtazamo wa kumdhalilisha mwanamke na kuongeza kuwa, ndani kabisa ya utamaduni wao, Wamagharibi wanamchukulia mwanamke kuwa ni bidhaa na njia ya kushibishia matamanio ya nafsi ya wanaume, na wanatumia suhula na uwezo wao wote kulifikia lengo hilo, lakini wakati huo huo wanataja uhuru na kuuhusisha na harakati yao hiyo ya uovu, iliyojaa mapungufu na upotoshaji kama ambavyo wanajaribu kuhalalisha pia jinai zao kama vile mauaji na kupora utajiri wa mataifa mengine ya dunia na kuzivamia kijeshi nchi nyingine na kuziingiza kwenye vita nchi nyingine kwa visingizio kama vya kupigania uhuru, haki za binaadamu na demokrasia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mtazamo wa Uislamu kwa mwanamke kuwa ni kinyume kabisa na mtazamo huo wa nchi za Magharibi na kusisitiza kuwa, Uislamu unamwangalia mwanamke kwa jicho la heshima sana, unampa mwanamke hadhi na utukufu wake na unamuona mwanamke kuwa ana utambulisho na shakhsia yake huru.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kutoka katika uzoefu uliofanikiwa wa kushiriki vilivyo wanawake bingwa, wasomi na waumini wa nchini Iran katika nyuga tofauti za kielimu, kisiasa na kiutawala na kuongeza kuwa: Katika mazingira ya Kiislamu, mwanamke hufanikiwa kukua kielimu, kukua shakhsia yake, kuimarika kimaadili na kisiasa na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kimsingi kabisa ya kijamii, lakini pia habadiliki bali anaendelea kubakia vile vile mwanamke na anaona fakhari kuwa hivyo.
Aidha amekutaja kusambaratika familia za Magharibi na kuongezeka idadi ya watoto wasio na utambulisho kuwa ni miongoni mwa matokeo ya mtazamo wa utamaduni wa Magharibi kuhusiana na mwanamke na kuongeza kuwa, Magharibi itapata vipigo vikubwa zaidi kutokana na suala hili hili, na pole pole kutaanza kushuhudiwa matokeo mabaya ya matukio ya kijamii yatakayopelekea kusambaratika vibaya zaidi jamii hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataja viumbe wawili yaani mwanamme na mwanamke kuwa wote wana sifa za pamoja za kibinaadamu kwa mujibu wa Uislamu na kuongeza kuwa: Mwanamke na mwanamme, kila mmoja ana nafasi na jukumu lake maalumu kulingana na sifa zake maalumu za kimaumbile, katika kuendeleza kizazi cha mwanadamu, kukikuza na kumpa utukufu mwanadamu pamoja na kuendeleza historia ya kiumbe huyo, na kwamba kati ya mwanamme na mwanamke, mwanamke ana jukumu kubwa na muhimu zaidi katika suala hilo, yaani kuzaa vizazi vipya zaidi vya mwanadamu.
Amesema, vigezo vya Uislamu kuhusiana na familia na mipaka yake ya mahusiano ya kijinsia inabidi navyo vichunguzwe na kuangaliwa kwa kuzingatia misingi hiyo hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kukuza na kutia nguvu nafasi ya mwanamke kwa mtazamo wa Kiislamu kuwa ni jukumu kubwa zaidi la wanawake bingwa, wasomi na wenye vipaji katika ulimwengu wa Kiislamu na huku akitoa ushahidi kutoka katika nafasi kuu na ya kimsingi ya wanawake wa Iran katika matukio ya miaka 33 iliyopita ameongeza kuwa: Nafasi ya wanawake katika matukio ya kijamii, mapinduzi mbali mbali na katika harakati nzima ya mwamko wa Kiislamu pia ni muhimu mno kwani wakati wowote mwanamke anaposhiriki katika harakati ya kijamii kwa muono mpana, basi ushindi wa harakati hiyo huweza kudhaminiwa na kwamba uhakika huo unalifanya jukumu la kutia nguvu uwepo na jitihada za wanawake katika matukio ya Misri, Libya, Bahrain, Yemen na kwenye maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu, kuwa jambo la lazima na la dharura kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mwamko wa Kiislamu uliojitokeza hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni harakati ya ajabu na isiyo na mfano na kusisitiza kuwa, harakati hiyo inaweza kubadilisha kabisa muelekeo wa hivi sasa wa historia ya mwanadamu lakini kwa sharti kwamba ijue vizuri masuala yanayoweza kuikwamisha na kukabiliana vilivyo na hatari na mambo mengine yote yanayoweza kuisambaratisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasifu mapinduzi ya wananchi katika mataifa ya Waislamu ya kaskazini mwa Afrika na kwenye maeneo mengine yanayoshuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Waistikbari wakiongozwa na Marekani na Uzayuni ambao wameshitukizwa vibaya na harakati hii adhimu, hivi sasa wanafanya juhudi zao zote kuidhibiti harakati hiyo na kuitumia vibaya kwa faida zao.
Amekutaja kupunguza hamu ya wananchi ya kuendelea kujitokeza kwenye masuala ya kupigania haki na kuwashuhgulisha watu wa matabaka mbali mbali ya wananchi wa nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na masuala ya kipuuzi au ya kuzusha hitilafu na mifarakano, kuwa ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na mabeberu wa dunia katika juhudi zao za kuudhibiti mwamko huo wa Kiislamu na kutahadharisha kuwa: Kama mataifa ya Waislamu hayatasimama imara na kidete katika kukabiliana na njama hizo na kama Waislamu wataendelea kuweko kwenye medani ya mapambano, basi ushindi wao dhidi ya ulimwengu wa kiistikbari utakuwa ni kitu cha lazima kwani nguvu za upanga za mabeberu wote huwa ndogo na hufeli mbele ya uwepo na imani ya kweli ya wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia njama na hatua zisizosita lakini zilizoshindwa za maadui wa Uislamu na maadui wa Iran katika kipindi cha miaka 33 iliyopita na kuongeza kuwa: Wamagharibi leo hii wanapiga makelele mengi kuhusu vikwazo dhidi ya Iran lakini hawajui kwamba vikwazo vyao ambavyo vinaendelea tangu miaka 30 iliyopita dhidi ya Iran vimelipiga chanjo ya kinga taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, taifa la Iran limefanikiwa kukabiliana vilivyo na njama na vikwazo vyote vya maadui kwa roho, mali na kutoa muhanga watu wake azizi na hivyo kufanikiwa kupata maendeleo makubwa katika kipindi hicho kiasi kwamba Iran ya leo hii siyo tena ile ya miaka 30 iliyopita bali imekuwa imara zaidi kwa mara mia moja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia maendeleo mbali mbali ya Iran katika nyuga tofauti na kuwakhutubu wanawake wasomi, bingwa na wenye vipaji wa ulimwengu wa Kiislamu akiwaambia: Leo hii mwanamke wa Kiislamu wa Iran anashiriki vilivyo katika nyuga zote kwa heshima na utukufu na kwamba wanawake wasomi na wenye vipaji wa Iran ni sehemu ya wanawake waumini zaidi na wanamapinduzi zaidi kati ya wanawake wa Iran na ndio maana Magharibi inatumia maelfu na njia za propaganda na makombora ya habari ili kujaribu kupotosha na kuonesha sura nyingine isiyo ya uhakika wa mambo kuhusiana na wanawake wa Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia njama zilizoshindwa za Magharibi za kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iachane na misimamo yake ya kuliunga mkono taifa la Palestina na kusisitiza kuwa: Sisi tofauti na mijadala ya upotoshaji kama vile ya Ushia na Usuni, siku zote tumesimama pamoja na ndugu zetu wote Waislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu limesimama pamoja na taifa la Palestina na matokeo yake mataifa yote yameamka na watu wote wanaokabiliana na Marekani na Uzayuni wamesimama imara na watu wengi wanawaunga mkono watu wanaokabiliana na mabeberu tena bila ya kumwogopa mtu yeyote wala dola lolote lile.
Katika mkutano huo, Bibi Hijazi, Katibu wa Kongamano la Kimataifa la Wanawake na Mwamko wa Kiislamu sambamba na kuashiria kushiriki wanawake 1200, wasomi na wanaharakati wa masuala mbali mbali kutoka nchi 85 tofauti dunia kwenye kongamano hilo, ametoa ripoti kuhusu masuala mbali mbali yaliyojadiliwa kwenye kongamano hilo na kwenye kamisheni maalumu za mkutano huo.
Naye Dk. Ali Akbar Velayati, Katibu Mkuu wa Halmashauri ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu ametoa hotuba fupi na huku akiashiria kufanyika makongamano manne ya kimataifa kuhusu mwamko wa Kiislamu tangu mwaka jana hadi leo hii amesema kuwa, lengo la Halmashauri ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu la kuitisha makongamano hayo ni kuifanya fikra ya mwamko wa Kiislamu izidi kupata nguvu na kwenda na wakati.
Mwanzoni mwa mkutano huo washiriki kadhaa wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Mwamko wa Kiislamu uliofanyika kwa muda wa siku mbili mjini Tehran -kutoka nchi tofauti duniani - wamepata fursa ya kutoa mitazamo na fikra zao kuhusu mwamko huo, mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
1050665