Muhammad Ridha Qazalsufla, mwambata wa Kiutamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sierra Leone amesema kwamba maana halisi ya kusubiri kudhihiri kwa Imam Mahdi (af) katika aya za Qur'ani na riwaya za Kiislamu ni kuwa na matumaini na mustakbali, jambo linalohuisha na kuleta mwamko, uchangamfu, utayarifu na maendeleo katika jamii ya Kiislamu.
Amesema maana hasi na isiyo sahihi ya kusubiri huko husababisha udhaifu na kusalimu amri mbele ya matukio mbalimbali katika jamii.
Mwambata huyo wa masuala ya kiutamaduni alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika kikao maalumu kilichofanyika huko Free Town chini ya anwani ya "Kusubiri, Mwamko na Ustawi wa Vijana." Wanachuo wa Kiislamu na Kikristo wapatao 200 walihudhuria kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Free Town.
Qazalsufla aliashiria baadhi ya aya na hadithi za Kiislamu na kusema kwamba viongozi wa kidini wa sasa na wa kale wamesisitiza juu ya nukta hii kwamba kusubiri kudhihiri kwa Imam Mahdi (af) kuna umuhimu mkubwa katika maisha ya mwanadamu na kuwataka Waislamu walizingatie suala hilo katika kipindi cha gheiba ya Imam huyo mtukufu. Amesema utayarifu wa kifikra, kiroho, kinafsi, kielimu, kimipango na kimkakati ni miongoni mwa nguzo muhimu za kusubiri huko na kwamba mwanadamu anayesubiri kudhihiri
kwa Imam Mahdi (af) anapasa kuandaa mazingira ya kuwepo uadilifu unaoandamana na elimu na teknolojia, udugu na haki katika jamii. 1054689